NA. DENIS CHAMBI, TANGA

Serikali imetoa kiasi cha shilingi Million 580 kwaajili ya ujenzi madarasa 29 ya Sekondari katika kata zilizopo ndani ya halmashauri ya jiji la Tanga  ambapo yanatakiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu na hatimaye kuanza kutumika kwa muhula mpya wa masomo wa mwaka 2023.

Mara baada ya kutoa fedha hizo serikali imeziagiza halmashauri zote nchini zilizopokea fedha kwaajili ya miradi hiyo kukamilika December 31, 2022 ambapo katika kuhakikisha mkoa wa Tanga unaendana na maagizo hayo mkuu wa mkoa Omari Mgumba  aliagiza Madara yote  yanayotekelezwa  na  fedha  hizo  yakamilike na kukabidhiwa November  15 mwaka huu. 

Akizungumza Mkurugenzi wa Halmashauri ya jiji la Tanga Dkt. Sipora Liana amesema kuwa katika kuhakikisha  wanatekeleza maagizo hayo na kutimiza adhima ya serikali tayari mchakato wa ujenzi wa miradi hiyo umeshaanza  kwa hatua ya za awali ikiwemo uchimbaji wa msingi kwa baadhi ya maeneo.

"Tuna miradi ya maendeleo ambayo Mheshimiwa Rais ametoa fedha kwakweli hatuna budi kumshukuru sana Rais wetu Samia Suluhu Hassan ametoa  shilingi mia tano themanini kwaajili ya ujenzi wa madarasa 29 yaliyopo ndani ya jiji la Tanga"

"Sasa hivi ndio tumeanza  utaratibu wa ujenzi wa madarasa na tayari baadhi ya madarasa misingi imeshaanza  kuchimbwa  na mengine tumeshaanza utaratibu wa kuwapata mafundi, matofali yameshaanza kusambazwa katika shule zote zinazojengwa kwenye shule za  Sekondari za Kiomoni, Ummy Mwalimu, Tanga ufundi, Hoten, Kirare, Marungu  pamoja na  Chongoleani na sasa hivi tunachoendelea nacho kote huko ni kupelekea vifaa vyote ili ujenzi uweze kuanza mara moja" alisema Dkt. Liana.

"Tumeweka timu za kusimamia hayo madarasa  tunanunua taa za kumulika ili kuhakikisha usiku na mchana  ujenzi unafanyika na tutahakikisha hatumuangushi Rais katika ujenzi huu" aliongeza.

Aidha Dkt Liana ameongeza kuwa wanaendelea kutoa mikopo ya asilimia 10 za mapato ya ndani kwa wakina mama, vijana na watu wenye ulemavu ambapo katika kipindi cha  robo ya nne ya mwaka wa fedha 2021/2023  wametoa zaidi ya  shilingi Million 300 kwa vikundi vya wajasiliamali.

Alisema katika kuhakikisha mikopo hiyo inawanufaisha walengwa halmashauri hiyo imejiwekea utaratibu wa kutoa elimu kwa vikundi vinavyopata mikopo hiyo  namna jinsi ya kuitumia vyema ili iwaletee maendeleo na hatimaye kufanya marejesho kwa wakati.

"Tuna utaratibu  pia  wa kuhamasisha vijana wakina mama na watu wenye ulemavu waweze kuja kuomba mikopo, wataalamu wetu tumewapanga  waweze kuwasaidia kupata mikopo hii isiyo na riba  tunahimiza wananchi wa Tanga  waje tutawapa mafunzo na kuwaelekeza namna ya kuomba hasa vijana tuna programu nyingi Sana tumeziandaa kwaajili yao,  ili vijana  wasitumike kwenda kwenye makundi ya kiuhalifu" alisema Liana

Akiwa katika kikao Cha baraza la Madiwani cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2022/2023 mstahiki meya wa jiji la Tanga Abdurahman Shillow amewataka Madiwani watendaji pamoja na viongozi wote katika kata zote zinazotekeleza miradi hiyo ya shule  kuhakikisha wanashirikiana kuisimamia kwenye  ujenzi  iuweze kuendana na kasi ili kukamilika kwa wakati.

" Sasa hivi tuna miradi ya madarasa 29  ambayo tumepata fedha  kutoka kwa Rais kwaajili ya kuepuka uhaba wa madarasa kwenye mwaka wa masomo wa 2023 niwaombe sana kuhakikisha madarasa hayo yanakamilika kama tulivyoelekezwa haya yatafanikiwa ikiwa sisi Madiwani  tutatoa ushirikiano wa kutosha lakini mahali popote kwenye changamoto basi sisi  tuanze kuzitatua kule kwenye  kata zetu" alisema Shillow

Aidha Shillow amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo pamoja na wataalamu wake kupata ufumbuzi wa haraka kwaajili ya ujenzi wa soko la Mlango wa chuma ikiwa ni pamoja na kuwahamasisha wafanyabiashara  wanaofanya biashara zao ndani ya solo hilo liweze kujengwa ambapo  halmashauri tayari imeshatoa shilingi Million 100 katika mradi huo.

" Miradi mingine inayoendelea kama ilivyo soko la Mlango wa Chuma  ninaomba mfikie ufumbuzi wa kudumu ili ijulikane wafanyabiashara wale wanakwenda wapi na soko lianze kujengwa  kwa sababu tumeshawekeza millioni Mia naomba Mkurugenzi wangu pamoja na wataalamu wako  muhakikishe ujenzi ule unaanza mara moja lakini na miradi mengine kasi ya ujenzi iongezeke" alisema Shillow.

Share To:

Post A Comment: