HIFADHI ya Taifa Ruaha imesema imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imekuwa ikiibuliwa na wananchi wa vijiji ambavyo vinazunguka hifadhi hiyo na moja ya mradi ambao umejengwa ni mradi wa Birika la Kunyweshea mifugo.

Akizungumza kuhusu miradi hiyo Ofisa Uhifadhi Hifadhi ya Taifa Ruaha kitengo cha Uhusiano kwa jamii Priscus Mrosso amesema kwa Wilaya ya Mbarali kitengo hicho kimetekeleza miradi mikubwa katika miaka ya karibuni na miradi hiyo ni Birika la Kunyweshea wanyama ambalo lipo Kijiji cha Nyeregete.

Pia kuna mradi wa Kisima cha maji katika shule ya sekondari ya Mbarali iliyopo Ubaruku na katika kijiji cha Mawindi kuna Bwalo la chakula pamoja na choo cha wanafunzi huku akifafanua miradi hiyo huwa inaibuliwa na wananchi kwenye vikao vyao vya kuibua miradi ya vijiji na hifadhi kama hifadhi inachangia asilimia 90 ya kufanikisha miradi hiyo.

“Baada ya vijiji kuibua hiyo miradi wanaandika barua kuleta hifadhini na kuomba hifadhi ichangie na hivyo hifadhi katika bajeti zake za mwaka inajadili na hatimaye inapelekwa makao makuu kwa ajili ya kuombewa fedha.

“Kwa huu mradi wa kijiji cha Nyeregete wa birika la kunyweshea mifugo unagharimu zaidi ya Sh.milioni 68 ambapo TANAPA kama TANAPA imechangia asilimia 90 na wananchi wanachangia asilimia 10, mradi wa kisima cha maji Sekondari ya Mbarali TANAPA imechangia asilimia 90 sawa na milioni 66 na wananchi nao wamechangia asilimia 10

“Katika kijiji cha Mawindi kwenye Shule ya sekondari Mawindi ambapo bwalo la chakula limejengwa pamoja na choo cha wanafunzi jumla ya Sh.milioni 162 zimetolewa na hifadhi na wananchi nao wamechangia kwa asilimia 10. Miradi hii yote iko mbioni kukabidhiwa Novemba mwaka huu ili wananchi waisimamie wenyewe,”amesema.

Akifafanua zaidi kuhusu mradi wa birika la kunyweshea mifugo Kijiji cha Nyeregete amesema wanategemea mifugo zaidi 1000 itakuwa inakunywa maji kila siku na lengo la mradi huo ni kupunguza wimbi la mifugo kuingia ndani ya hifadhi kunywa maji katika mito iliyoko ndani ya hifadhi.

“Tunafahamu Mto Ruaha ni tegemeo kwa hifadhi ya Ruaha na taifa kwa ujumla, kwa hiyo kwa kujenga hili birika la kunyweshea mifugo itapunguza kwa asilimia kubwa mifugo kuingia ndani ya hifadhi kunywa maji na kuharibu vyanzo vya maji ambavyo vinaingia mto ruaha.

“Mto Ruaha unamanufaa makubwa katika nchi yetu kwani unaanguna na Mto Kidatu na Mto Rufiji kwenda kuingiza maji kwenye bwawa kubwa la Mwalimu Nyerere ambalo Serikali inatumia fedha nyingi kutengeneza mradi wa kufua umeme wa megawati 2115.”

Alisema awali mifugo mingi ilikuwa inaingizwa ndani ya hifadhi na inakwenda kuharibu vyanzo vya maji lakini baada ya mradi huo mifugo imepungua na kufanya kuwepo na utulivu ndani ya hifadhi ya Ruaha.

Amesema mifugo ambayo ilikuwa inaingia ndani ya hifadhi ya kabla ya birika kujengwa ni zaidi ya ng’ombe 5000 walikuwa wanaingia hifadhini kwa ajili ya kunywa maji kwa siku kutoka kwenye vijiji tofauti lakini birika ambalo limejengwa sasa ni maalumu kwa ajili ya kijiji cha Nyeregete.

Aidha amesema vijiji vingine ambavyo vitaomba mradi kama huo vinaweza navyo kujengewa lakini itategemea na bajeti ya hifadhi iliyopo kwa wakati huo.

Kwa upande wa wananchi wamesema wanaishukuru Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa kukamilisha mradi huo wa maji kwa ajili ya kunyweshea mifugo na kwamba huko nyuma walikuwa wanapata shida kubwa ya kutafuta maji kwa ajili ya kunyweshea mifugo.

Mmoja ya wananchi Albert Msengwa amesema walikuwa wanachimba visima lakini hawapati maji, hivyo wakawa wanakwenda ndani ya hifadhi kwa ajili ya kutafuta maji lakini kupitia mradi huo hivi sasa wanapata maji.

“Tunashukuru sana na sasa hivi hatutaenda tena kwenye hifadhi kwa ajili ya kufuata maji, malisho tunayo na maji tunayo.Ni raha sana , tunashukuru maji mazuri ng’ombe wanakunywa na sisi wananchi tunakunywa maji haya haya,”amesema.

Kwa upande wake Mkazi wa Kijiji cha Nyeregete John Mjengwa amesema wanaishukuru TANAPA na wanaishawishi hata vijiji vingine ambavyo vimezunguka hifadhi ya Taifa vipatiwe miradi kama huo ili kuondokana na msongamano wa kuingia ndani ya hifadhi.

“Tunafahamu jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan hivyo tunaomba aendelee kujitolea ili vijiji vingine navyo viwe na mradi kama huu na hapo tutakuwa tumepunguza wana vijiji kuingia kwenye hifadhi.

“Awali wale wenye ng’ombe nyingi ndio walikuwa wanaingia hifadhani , kwa kweli Rais ametuokolea eneo kubwa na tunaamini kwa sasa ng’ombe hawawezi kuingia tena ndani ya hifadhi.”

Baadhi ng'ombe wakinywa maji kwenye Birika maalum la kunyweshea maji mifugo ambalo limejengwa na Hifadhi kwa ajili ya kutatua changamoto ya upatikani wa maji kwa Wafugaji wanaoishi katika kijiji cha Nyeregete ikiwa ni sehemu ya mradi wa Ujirani mwema uliojengwa kwa gharama ya shilingi milioni 68,ambapo Hifadhi imechangia mradi huo kwa aislimia 90 lakini na Wananchi nao wamechangia asilimia 10
Mmoja wa Wakazi wa kijiji cha Nyereregete akichota maji katika mradi wa maji wa ujirani mwema uliojengwa na Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kwa wanakijiji cha Nyeregete,mkoani Iringa kupunguza changamoto ya upatikanaji wa maji kwa wakazi wa kijiji hicho kinachoizunguka Hifadhi.
Ofisa Uhifadhi Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kitengo cha Uhusiano kwa jamii Priscus Mrosso akizungumza na baadhi ya Wakazi wa kijiji cha Nyereregete ambao wananufaika na mradi wa ujirani mwema wa Kisima cha maji uliojengwa na Hifadhi







 Ofisa Uhifadhi Hifadhi ya Taifa ya Ruaha kitengo cha Uhusiano kwa jamii Priscus Mrosso akizungumza na baadhi ya Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Mbarali iliyopo Ubaruku waliokuwa wakichota maji kwa ajili ya matumizi yao shuleni hapo

Mradi wa Bwalo la Chakula pichani juu na Choo cha Wanafunzi pichani chini vilivyojengwa katika Shule ya Sekondari ikiwa katika hatua za mwisho kukamilika,ambapo jumla ya Sh.milioni 162 zimetolewa na hifadhi na wananchi nao wamechangia asilimia 10.
Share To:

Post A Comment: