Na Christina Thomas, Morogoro


BODI ya maji Bonde la Wami Ruvu katika kulinda vyanzo vya maji imelazimika kusitisha vibali 12 vya watumiaji maji mkoani Morogoro ili kupunguza matumizi ya maji na kukabiliana na hali ya ukame iliyopo inayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.

Mkurugenzi wa Bodi ya maji Bonde la Wami Ruvu Elibariki Mmassy alisema hayo jana kwenye kikao cha wadau wa maji wakiwemo wa viwanda, umwagiliaji, na Wavuvi ambapo alisema katika kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa maji wameamua kusitisha jumla ya vibali 12 na hali ikirudi kama kawaida wenye vibali wataendelea na shughuli zao.

Mmassy alisema bodi tangu mwezi wa Mei ilishatoa barua kwa wadau wake juu ya kutokuwepo kwa mvua za kutosha za masika na vuli na kuwataka kutowekeza kutokana na maji kutotosheleza.

Hivyo aliwataka wadau wa maji kuzingatia vipaumbele vya utoaji wa vibali ikiwemo utunzaji wa mazingira, matumizi ya majumbani na kulingana na upatikanaji maji ambapo alisema kupunguza matumizi ya maji kutasaidia kupambana na upungufu wa maji ikiwemo kuacha shughuli za kumwagilia ikiwemo maua majumbani.

Mkurugenzi huyo alisema ifaamike kuwa hali hiyo kwenye mzunguko wa maji huwa inatokea na ndio maana Rais Samia Suluhu Hassan aliwekeza kujenga bwawa la Kidunda ambalo linakaribia kufanya kazi ambapo Waziri wa maji Juma Aweso ametoa kipaumbele cha ujenzi wa mabwawa madogo madogo matano kwenye safu za milima ya Uluguru yatakayobea kiasi cha maji ya mita za ujazo kuanzia mililita 19 mpaka 21 ili kupunguza changamoto iliyokuwepo.

Alisema mwaka huu haukuwa  na mvua toshelevu na kufanya kupungua kwa kina cha maji kwenye mito mingi ambapo mpaka sasa kuna na maji lita 2580 kwenye mto huku mililita 1870 zikiwa kwenye mto Wami ambapo mahitaji ya maji ya kiujumla ni lita 9000 na mahitaji ya majumbani ni lita 5800.   .

 “miaka ya kawaida kwa tarehe kama ya leo kunakuwa na ujazo wa mililita 14,000 kwenye mto lakini kutokana na mabadiliko ya tabianchi, na kutokuwepo na mvua za kutosha za masika na vuli, na ukame katika mwezi huu wa Oktoba hali imekuwa tofauti, na hali kama hii hutokea mwezi wa Novemba mwishoni wakati mvua za masika zinaanza kunyesha na kufanya kutokuwa na shida ya maji” alisema Mkurugenzi huyo

Aidha alisema wanategemea kuwa na mvua kiasi wiki ya tatu ya mwezi Desemba ambayo wanadhani inaweza kusaidia huku wakiwa wameshatoa taarifa kwa wadau za maeneo yanayofaa kwa uchimbaji wa maji ya visima kwenye maeneo ya Dar es salaam, Morogoro na Dodoma.

Mmassy alisema kutokana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi pamoja na kuchelewa kwa mvua za vuli wameitana na wadau wa maji na kuwa na mikakati na makubaliano mbalimbali hasa katika kutunza vyanzo vya maji na kuhakikisha wanakabiliana na changamoto zote za maji.

Alisema katika kikao hicho wamejadili mambo mengi yenye nia chanya ya kujenga na kuhifadhi vyanzo vya maji kwenye bonde hilo kwa njia ya kushirikiana kwenye kutunza na uwekaji wa mipaka kwenye vyanzo vya maji na kuwekeza kwenye miundombinu ya kutunza maji kipindi cha masika.

Alisema kwa wadau wa wafugaji  nao waliendelea kuwapa taarifa huku wakijenga mabirika 6 yanayogharimu kiasi cha sh mil 60 na matano yakiwa kwenye Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro kama mfano kwa wafugaji kuweza kujenga wenyewe hasa kwa wale wenye ng’ombe wengi kuanzia 1000 na kuendelea anauwezo wa kujenga kwa ajili ya kupata maji na malisho.  

Share To:

Post A Comment: