WASTANI wa Watanzania  33,000 hufariki kila mwaka, kutokana na moshi wa kupikia.

Waziri wa Nishati January Makamba alisema hayo jana jijini Dodoma, wakati wa semina ya kuwajengea uwezo Wabunge wanawake kuhusu matumizi ya nishati mbadala nyumbani.

Makamba ambaye yuko nje ya nchi kikazi, alitoa ujumbe huo mbao ulirekidiwa kabla ya kusafiri.

“Nilitamani kuhudhuria semina hii, lakini nimepata safari niko nje ya nchi,  lakini kabla sijaondoka nilisema nitaacha rekodi ya ujumbe wangu,” alisema.

Alisema kuwa wastani wa Watanzania 33,000  wanakufa kila mwaka, kutokana na moshi wa kupikia  kwa kuugua magonjwa ya mfumo wa hewa.

Alisema matumizi ya nishati mbadala yataokoa  maisha ya kinamama na wote wanaotumia kuni.

“Saa moja kwenye jiko lenye  moshi ni sawa na kuvuta sigara 300, ukimpima mwanamke  wa Kijijini kwa X-ray  ni kama mtu aliyevuta sigara muda mrefu, ule moshi ambao ni sumu unaofanya hata wadudu wasikae jikoni ndio unaingia kwenye mapafu,” alisema.

Alisema kuwa hiyo inonesha wanawake Tanzania wanameza moshi unaowaua taratibu.

” Madhara mengine ni watoto kuzaliwa njiti  na mimba zinazotoka, ule moshi wa kupikia madhara yake hayazunguzwi sana, tunatakiwa kuchukua hatua. zinazostahili katika kumkomboa na kumsaidia mwanamke,” alisema.

Naibu Spika, Mussa Zungu alisema kuwa, matumizi ya kuni yamekuwa na madhara makubwa.

“Mlima Kilimanjaro unapoteza barafu kutokana na miti kukatwa, milima ikiishiwa barafu  hakutakuwa na utalii tena,” alisema.

Mkurugenzi wa Masoko na Uendelezaji wa Teknolojia, Mhandisi Advera Mwijage, alisema kuwa wanahamasisha matumizi ya nishati vijijini.

Share To:

Post A Comment: