WANAFUNZI  471 wa darasa la awali na la kwanza wa Mtaa wa Tulieni, Kata ya Nsemulwa, Manispaa ya Mpanda, mkoani Katavi, wameepukana na adha ya kutembea umbali mrefu wa zaidi ya kilomita nane kwa siku kwenda shule ya msingi Nsemulwa, baada ya shule shikizi ya Tulieni kuanza kutumika.

Hata hivyo shule hiyo inabiliwa na changamoto mbalimbali, hivyo wadau kuombwa kusaidia kuzitatua changamoto hizo.

Shule hiyo shikizi ya Tulieni ina jumla ya vyumba vinne vya madarasa na ofisi moja yenye walimu wawili.

Akizungumza na HabariLeo, mmoja wa walimu wanaofundisha shule hiyo, Alexander Semi,  amesema changamoto zinazoikabili shule hiyo ni pamoja na kuwa na matundu machache ya vyoo, ambapo yapo matundu manne pekee.

Changamoto nyingine ni upungufu wa samani kama madawati kwa wanafunzi, meza, viti, na makabati katika ofisi ya walimu, huku changamoto kubwa ikiwa ni kukosekana kwa huduma ya maji.

Amesema hali hiyo inawafanya kuwaagiza watoto kuja na maji shuleni, ambayo hata hivyo hayatoshelezi usafi kutokana na ukweli kwamba maji wanayobeba ni kwenye chupa za maji na huishia kusaidia mwanafunzi kunywa.

Amesema kuwa bado hawajaanza utaratibu wa kuwapikia watoto chakula shuleni, kutokana na mazingira magumu yaliyopo.

Mwalimu Said Mbogo ni mkuu wa shule ya msingi, Nsemulwa ambaye pia ni msimamizi wa shule shikizi ya Tulieni, amesema licha ya kufunguliwa kwa shule hiyo, bado ina changamoto kadhaa na kuomba watu mbalimbali kujitokeza kuisaidia kukamilika na hatimaye isajiliwe na kuwa shule ya msingi Tulieni.

Amesema Mtaa wa Tulieni unaendelea kuongezeka watu wanaojenga na kuishi maeneo hayo, hali inayoashiria kuwa ni lazima kuwepo na shule kwa ajili ya kuhudumia wanafunzi, huku akiwaomba watu wenye mapenzi mema kujitolea kwa hiari kuchangia ujenzi wa shule hiyo.

Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa Tulieni, wamesema shule hiyo imesaidia kuinua mwamko wa wazazi kuwaandikisha watoto shule, kwani kwa kutegemea shule ya Nsemulwa peke yake, ilikuwa ni vigumu kutokana na umbali uliopo hasa kwa watoto wadogo.

Share To:

Post A Comment: