Na,Moses Mashalla,


Zaidi ya wafanyabiashara 5,000 wanaofanya biashara katika soko la Samunge jijini Arusha wanataraji kupatiwa mitaji ya kuendesha biashara zao na mhubiri maarufu nchini Nabii Mkuu Dkt GeorDavie.

Mbali na kupatiwa mitaji hiyo pia mhubiri huyo anataraji kutoa msaada wa kukarabati miundombinu ya malango ya kuingilia ndani ya soko hilo kama njia mojawapo ya kusaidia jamii.

Akizungumza na waandishi wa habari mwenyekiti wa wafanyabiashara wa soko la Samunge,Joram Miraji amesema kuwa uongozi wa soko hilo hivi karibuni ulimwandikia barua ya maombi ya kuwasaidia mitaji wafanyabiashara ndani ya soko hilo pamoja na kusaidia kukarabati miundombinu ambapo ombi lao limekubaliwa.

Miraji amesema kuwa baadhi ya wafanyabiashara ndani ya soko hilo hawana mitaji kufuatia soko hilo kuungua mwaka 2019  na kuteketeza mali zao.

Mwenyekiti huyo amesema kuwa wafanyabiashara wengi ndani ya soko hilo wanaishi kwa mateso kufuatia kudaiwa mikopo na baadhi ya benki nchini hali ambayo imepelekea kero na usumbufu kwa uongozi wao.

Miraji amesisitiza kuwa hatua ya kumuandikia barua Nabii Mkuu Dkt GeorDavie imekuja baada ya kuona anasaidia makundi mbalimbali kwenye jamii hivyo na wao waliona wamuandikie barua na tayari wameshapatiwa majibu kuwa atawatembelea.

Naye mweka hazina wa soko hilo ,Amos Julius amesema kwamba soko lao linakabiliwa na changamoto ya miundombinu hususani malango ya kuingilia na kupelekea baadhi ya wafanyabiashara kuibiwa bidhaa zao.

“Soko liko wazi sana na hii imepelekea baadhi ya wezi kupenya na kuchukua bidhaa za wafanyabiashara hivyo tunamuomba Nabii Mkuu Dkt GeorDavie atusaidie katika hili “amesema Julius 

Mfanyabiashara Upendo Remy amesema kuwa pindi moto ulipounguza soko hilo alijikuta akipata hasara ya sh 500,000 na sasa anaishi kwa mikopo.

Naye Agripina Kawalla amesema kuwa wanakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa mitaji ya kuendesha biashara zao na endapo Nabii Mkuu Dkt GeorDavie akiwashika mkono watainuka kiuchumi.

Hivi karibuni akiwa katika ibada katika huduma yake ya Ngurumo ya Upako Nabii Mkuu Dkt GeorDavie alitoa kauli ya kufanya ziara ya kutembelea soko la Samunge na kuwasaidia changamoto mbalimbali kama mitaji wafanyabiashara waliopo ndani ya soko hilo.

Share To:

JUSLINE

Post A Comment: