Na Joachim Nyambo,Mbeya.


MTOTO wa kiume anayekadiriwa kuwa na umri wa mwaka mmoja na miezi tisa ametelekezwa na mama yake mzazi nyumbani kwa mkazi wa Mtaa wa Mwasote uliopo katika Kata ya Itezi jijini Mbeya.


Mwanamke aliyetelekezewa mtoto huyo anafahamika kwa jina la Imelda Mwansasu wakati mama mtelekezaji wa mtoto inadaiwa alijitambulisha kwa jina moja tena kwa kifupi la Mage huku mtoto aliyetelekezwa akiwa na uwezo wa kujitaja jina lake moja pekee la Vicent.


Kwa mujibu wa Imelda mnamo Novemba tisa mwaka huu majira ya saa nane mchana akiwa amejipumzisha kwa kujilaza chumbani nyumbani kwake mlango wa nche wa nyumba yake ulibishwa hodi na mwanamke aliyejitambulisha kwa jina moja la Mage.


Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jana Imelda alisema mwanamke huyo aliyebisha hodi baada ya kukaribishwa na mwenyeji alijieleza kuwa anakwenda maeneo ya jirani hivyo akaomba amwache mtoto nyumbani hapo akidai si muda mrefu angerudi kumchukua lakini ajabu alitokomea hata kabla mwenyeji hajatoka nje ili waweze kutambuana.


Mwenyeji huyo alisema mara baada ya kutoka nje ya nyumba yake mlangoni hakumkuta mgeni aliyebisha hodi na badala yake alimkuta mtoto huyo  na pembeni yake kukiwa na kifungashio ambacho mara baada ya kukikagua ndani yake akakuta kisepe(nepi) kimoja,suruali moja na kontena la plastiki lililokuwa na wali usiokuwa na mboga.


Anasema mazingira hayo yalianza kumpa mashaka kiasi lakini akajipa moyo na kuamini huenda maneno aliyoambiwa yana ukweli na kwamba huenda mhusika alikuwa na haraka kiasi cha kushindwa kusubiri mpakamwenyeji atoke ili amkabidhi huku imani nyingine ikiwa kuna uwezekano wa mgeni huyo kuwa na uhakika wa eneo analomwacha mtoto.


Lakini kadiri muda ulivyozidi kwenda hali ilionekana kuwa tofauti na ndipo ikamlazimu msamaria mwema huyo kuanza kuhaha kwa majirani kuulizia mtoto aliyeachiwa ni wa nani na baada ya kuona kila anayeulizwa akawa hamjui ndipo akabaini kuwa alitelekezewa.


Aliongeza kuwa baada ya kujadili na majirani ikawalazimu kuushirikisha uongozi wa mtaa kwakumfikisha mtoto huyo nyumbani kwa balozi ili apate usaidizi huku hofu zaidi ikiwa ni iwapo mtoto huyo atapatwa na matatizo au ana changamoto zozote za kiafya.


“Tokea alipomuacha hakurudi tena hivyo hatuelewi ndugu zake ni akina nani.Tuna hofu kwa lolote litakalomkuta baadaye ikawa ni shida kwetu.Jina lake alisema anaitwa Mage na alisema tu kuwa anakaa hapo Jelele ila sasa hatuelewi kila tunayejaribu kumuuliza anasema hamfahamu.” Alielezea Imelda ambaye mpaka sasa analazimika kuendelea kuishi na mtoto.


Kwa umri alionao mtoto huyo,anastahili kuendelea kuhudhuria kliniki kama inavyofanyika kwa watoto wengine lakini kwa mujibu wa maelezo ya Imelda kwenye kifungashio kilichokuwa na vitu vyake hakukuwa na kadi ya kliniki wala cheti kinachoonesha historia ya maendeleo ya kiafya ya mtoto husika.


Mwenyekiti wa mtaa wa Mwasote,January Robert alisema alipata taarifa za mtoto huyo kutoka kwa balozi wake aliyemtaja kwa jina moja la Benard baada ya kumaliza mkutano wa hadhara uliofanyika mtaani hapo.


Alisema baada ya kupewa taarifa hizo za kutelekezwa kwa mtoto aliamua kuwarudisha mkutanoni tena wananchi na kuwaelezea juu ya tukio hilo lakini bado jitihada za kumpata mama husika hazikuzaa matunda na hapo wakaamua kutoa taarifa kwa jeshi la polisi.


Sikujua Tembela ni mmoja wa majirani wa Imelda ambapo alisema kitendo kilichofanywa na mama wa mtoto huyo ni cha kikatili huku akisema kawa asili ya wanawake wa Mkoa wa Mbeya walivyowapambanaji pamoja na uwepo wa changamoto zinazomkabili angeweza kumlelea mwanaye.


Mpaka sasa mtoto yupo nyumbani kwa msamaria huyo na yeyote anayemfahamu mama mwenye mtoto anaweza kuwasiliana na Imelda kwa namba 0742 267 764.

Share To:

JUSLINE

Post A Comment: