Na. Veronica E. Mwafisi-Dodoma

Tarehe 25 Septemba, 2022

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na

Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ameitaka Kamati ya Taifa ya

Uongozi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuwa na utamaduni wa

kuwatembelea walengwa wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini,

unaoratibiwa na TASAF ili kubaini na kuzitafutia ufumbuzi changamoto

zinazoweza kukwamisha utekelezaji wa mpango huo ambao Serikali

inautekeleza kwa lengo la kuboresha maisha ya kaya maskini nchini.

Mhe. Jenista ametoa maelekezo hayo jijini Dodoma, wakati akizindua

Kamati ya Taifa ya Uongozi ya TASAF iliyoteuliwa hivi karibuni mara baada

ya kamati iliyopita kumaliza muda wake kiutendaji.

Waziri Jenista amewahimiza wajumbe wa kamati hiyo, kuhakikisha

wanakwenda kuzungumza na viongozi, waratibu na walengwa katika

maeneo yote ambayo Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unatekelezwa,

ili kufikia lengo la Serikali la kuzikwamua kaya maskini kutoka katika lindi la

umaskini.

“Mhe. Mwenyekiti na wajumbe wa kamati hii, tembeleeni maeneo ambayo

mpango wa TASAF unatekelezwa ili mjiridhishe namna ambavyo

unawafikia walengwa na kuwanufaisha,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa, wajumbe wa kamati wakitembelea maeneo

ambayo mpango wa TASAF unatekelezwa, watapata fursa ya kujionea

namna walengwa walivyonufaika, ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto

ambazo walengwa hao wa TASAF wanakabiliana nazo.

Akizungumzia azma ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuzikwamua kaya

maskini, Mhe. Jenista amesema kuwa Serikali chini ya uongozi wa Rais wa

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan

haitomuacha mtu nyuma katika kufikia malengo ya maendeleo kama

yalivyoainishwa katika dira ya maendeleo (Vision 2025), na ndio maana


imejipanga vema katika kuhakikisha inaboresha maisha ya kaya zote

maskini kwenye vijiji, mitaa na shehia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Peter Ilomo

amemhakikishia, Mhe. Jenista kuwa yeye pamoja na kamati yake

watayafanyia kazi maelekezo yote ambayo ameyatoa ili kutimiza lengo la

serikali la kuboresha maisha ya kaya maskini.

Naye, Mwenyekiti aliyemaliza muda wake, Dkt. Moses Kusiluka amesema,

ataendelea kushirikiana na TASAF ili kuhakikisha inatimiza lengo lake la

kuboresha maisha ya wananchi ambao wanaishi katika familia zenye hali

duni kiuchumi.

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya taasisi yake,

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Bw. Ladislaus Mwamanga amesema,

TASAF imekuwa na mafanikio makubwa katika kuboresha maisha ya kaya

maskini ikiwa ni pamoja na kujenga rasilimaliwatu ya kutosha kwa

kuwawezesha kielimu wanafunzi wanaotoka kwenye kaya maskini kutoka

hatua moja kwenda nyingine.

“Mwaka jana, TASAF kwa kushirikiana na bodi ya mikopo tumewawezesha

wanafunzi 1200 kujiunga na elimu ya juu katika vyuo vikuu mbalimbali

nchini, na mwaka huu mchakato bado unaendelea lakini tunatarajia

kuwawezesha wengi zaidi kwani walioomba wako zaidi ya 3000,” Bw.

Mwamanga amefafanua.

Kamati ya Taifa ya Uongozi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF)

kwa sasa inaundwa na Mwenyekiti Bw. Peter Ilomo, pamoja na wajumbe

wengine ambao ni Balozi Zuhura Bundala, Bw. Richard Shilamba, Dkt.

Charles Mwamwaja, Dkt. Ruth Lugwisha, Dkt. Naftali Ng’ondi, Bw. Ali

Salim Matta, Mhandisi Rogatus Mativila na Dkt. Grace Magembe.

Share To:

Post A Comment: