Pamoja na shughuli ya kuhesabu watu ikiendelea katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, changamoto ya umeme inasababisha baadhi ya maeneo sensa ya watu na makazi kuendelea kwa kasi ndogo.

Mratibu wa sensa wa Wilaya ya Simanjiro Linus Mboya akizungumza na Mwandishi wetu wa Habari leo Jumatano Agosti 24 amewatoa hofu wana Simanjiro kuwa wote watafikiwa kwani watahesabiwa kwa muda wa siku saba.

"Wana Simanjiro wasihofu watahesabiwa wote kwani baadhi ya vishkwambi havina power bank na maeneo mengine hakuna umeme wa kuchaji ndiyo sababu kunakuwa na kasi ndogo ila watafikiwa wote," amesema Mboya.

Hata hivyo, amesema tangu shughuli hiyo ianze imefanyika inavyopaswa hakuna kishkwambi kilichopotea wala makarani wa sensa kuwa walevi hivyo wanatimiza wajibu wao ipasavyo.

Mkazi wa kijiji cha Shambarai Obeid Sarakikya amesema jana Agosti 23 alishinda nyumbani kwake akiwasubiri makarani wa sensa ili ahesabiwe ila hawakufika.

Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Shujaa Baruti amesema jana hakuhesabiwa ila anasubiria kwani wameelezwa itafanyika kwa muda wa siku saba.

Share To:

Post A Comment: