Naibu Waziri wa Maji Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Mahundi,akiwa na timu ya wataalamu ya wizara hiyo wakitembelea na kujionea Malaka ya Maji ya Taifa ya Zimbabwe (Zimbabwe National Water Authority – ZINWA) ambapo walipokelewa na kupewa maelezo namna ZINWA ilivyoanza utekelezaji wa ushirikishwaji wa sekta binafsi na matumizi ya dira za maji za malipo kabla ya matumizi.


Kushoto Mhe. Maryprisca Mahundi Naibu Waziri - Maji, Kulia ni Prof. Emmanuel Mbennah Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe aliyemaliza muda wake ambapo sasa nafasi yake itachukuliwa na Kamanda Simon Sirro.

....................................

Harare, Zimbabwe

Naibu Waziri wa Maji Mheshimiwa Mhandisi Maryprisca Mahundi ameongoza timu ya wataalamu kutembelea nchi ya Afrika Kusini na Zimbabwe ili kujifunza namna nchi hizo zinavyoshirikisha sekta binafsi katika kusimamia miradi ya maji vijijini sambamba na utumiaji wa dira za maji za malipo kabla ya matumizi.

Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Benki ya Dunia pamoja na RUWASA wanakamilisha upembuzi yakinifu wa ushirikishwaji wa Sekta binafsi na Matumizi ya Dira za Maji za Malipo Kabla ya Matumizi katika skimu za maji vijijini.

Akiwa nchini Zimbabwe Mhandisi Maryprisca na msafara wake walitembelea Malaka ya Maji ya Taifa ya Zimbabwe (Zimbabwe National Water Authority – ZINWA) ambapo walipokelewa na kupewa maelezo namna ZINWA ilivyoanza utekelezaji wa ushirikishwaji wa sekta binafsi na matumizi ya dira za maji za malipo kabla ya matumizi.

Pia walitembelea Bwawa la maji la Chivhu, mtambo wa kusafishia maji wa Chivhu na baadae wananchi wanaotumia dira za maji za malipo ya kabla ya matumizi katika kata ya chivhu mjini Wilaya ya Chikomba jimbo la Mashona Mashariki.

Akitoa uzoefu wa namna ZINWA ilivyoanza utekelezaji, Afisa mtendaji Mkuu wa ZINWA Mhandisi Taurayi Maurikio amesema, mchakato wa matumizi ya dira za maji za malipo kabla ya matumizi ulianza mwaka 2016 kufuatia changamoto za malipo ya ankara za maji kwa utaratibu wa malipo ya baada ya matumizi.

Pia alisema kuwa awali wananchi na viongozi wa seikali hawakupenda matumizi ya dira hizo, hata hivyo, baada ya kuonesha ufanisi mkubwa kwa sasa wananchi na seirikali wanapenda matumizi ya dira hizo kwa kuwa zimeonesha ufanisi mkubwa na uhalisia katika ankara za maji na kuepusha ukadiriaji wa malipo ya maji kutokana na changamoto za kutokusomwa au mapungufu ya wasomaji wa dira za maji.

Akihitimisha ziara yake Mheshimiwa Mhandisi Mahundi amesema, elimu waliyoipata na itawasaidia katika kukamilisha mchakato wa mradi wa ushirikishwaji wa sekta binafsi na matumizi ya dira za maji za malipo kabla ya matumizi nchini Tanzania.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Usambaji wa maji na usafi wa mazingira wa RUWASA Mhandisi Mkama Bwire amesema, serikali imefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika ujenzi wa miradi ya maji vijijini, hivyo changamoto imebaki namna serikali itaifanya miradi hiyo kuwa endelevu. “Ziara hii italeta manufaa makubwa nchini kwetu kwakuwa itakwenda kutusaidia kama nchi kwenye upande wa kuzifanya skimu zetu za maji vijijini kuwa endelevu” alisema Bwire.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: