Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akikata utepe kuashiria kuzindua Huduma za Mawasiliano ya Intaneti kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika kituo cha Horombo kilichopo katika Mlima Kilimanjaro jana Agosti 16, 2022. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mhandisi Peter Ulanga na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mohammed Khamis Abdulla (wa nne kutoka kushoto)

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akishiriki mkutano kupitia njia ya video na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. John Mongela baada ya kuzindua Huduma za Mawasiliano ya Intaneti kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika kituo cha Horombo kilichopo katika Mlima Kilimanjaro.


 Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akizungumza wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Huduma za Mawasiliano ya Intaneti kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika kituo cha Horombo kilichopo katika Mlima Kilimanjaro jana Agosti 16, 2022.


 Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akisisitiza jambo wakati wa uzinduzi huo.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akizungumza na wadau mbalimbali mara baada ya kuwasili Horombo Hut kwa ajili ya kuzindua huduma za Mawasiliano ya Intaneti yaliyofikishwa katika Mlima kilimanjaro na Shirika la TTCL

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye akiangalia mandhari nzuri katika Mlima Kilimanjaro wakati wa uzinduzi huo. Kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mhandisi Peter Ulanga.

Safari baada ya uzinduzi huo ikiendelea.

Picha ya pamoja baada ya uzinduzi huo.

 

Na Mwandishi Wetu, WHMTH, KILIMANJARO

 

WIZARA ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kupitia Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) imefikisha huduma ya mawasiliano ya intaneti yenye kasi katika Mlima Kilimanjaro.

Mlima huo mrefu zaidi barani Afrika, unaopatikana katika Mkoa wa Kilimanjaro nchini Tanzania umefikishiwa mawasiliano ya intaneti yenye kasi ili kuendelea kukuza Sekta ya utalii na upatikanaji wa huduma za kidijiti katika mlima huo.

Hayo yamezungumzwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye katika hafla ya uzinduzi wa huduma za mawasiliano ya intaneti katika Mlima huo iliyofanyika katika kituo cha Horombo cha Mlima Kilimanjaro, jana Agosti 16, 2022.

Alisema  kuwa huduma ya intaneti yenye kasi imefika katika kituo cha Mandara chenye umbali wa mita 2700, Kituo cha Homboro mita 3720 na Kituo cha Kibo mita 4720 juu ya usawa wa bahari huku matarajio ni kufikisha umbali wa mita 5895 katika kilele cha Uhuru ifikapo mwezi Desemba 2022.

Waziri Nape amezungumzia ufikishaji wa huduma ya intaneti yenye kasi katika mlima Kilimanjaro kuwa ni tukio la kihistoria kwa nchi ya Tanzania na bara zima la Afrika kwa kufungua fursa ya watalii na waongoza utalii kufanya mawasiliano ya mubashara na ndugu na familia zao wakiwa katika mlima huo.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu amesema kuwa Mhe. Rais Samia ameifungua sekta ya utalii nchini na Serikali anayoiongoza kupitia Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imeweka mazingira wezeshi ya sekta ya utalii kukua zaidi kwa kufikisha huduma ya intaneti ya kasi katika Mlima Kilimanjaro.

Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mohammed Khamis Abdulla amelipongeza Shirika la TTCL kwa kutatua moja ya changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa huduma za mawasiliano katika maeneo ya hifadhi na kulitaka Shirika hilo kuyafikia maeneo mengi zaidi.

Aidha, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mhandisi Peter Ulanga amesema kuwa mradi huo wa kufikisha mawasiliano ya intaneti yenye kasi katika mlima Kilimanjaro kwa gharama ya milioni 146 utekelezaji wake haukuwa rahisi lakini umewezekana kutokana na ushirikiano Mkubwa walioupata kutoka katika Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (TANAPA) na Mamlaka ya Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA).

 

Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari. 

Share To:

dottomwaibale

Post A Comment: