Julieth Ngarabali, Pwani, 


Serikali ya Tanzania na ya Jamuhuri ya watu wa Cuba zimetiliana saini mikataba miwili , mmoja wa miaka 10 ya uzalishaji mbolea hai (Biofertilizers) na mwingine wa miaka mitano wa uendeshaji kiwanda cha kuzalisha bidhaa za kibaolojia (Tanzania Biotech products ltd) cha Kibaha Mkoani Pwani.


Hafla hiyo imefanyika kwenye viwanja vya kiwanda hicho mjini Kibaha Mkoani Pwani baina ya pande hizo mbili na kushuhudiwa na Waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki Liberata Mulamula.


Akizungumza kwenye hafla hiyo Mulamula amesema tukio hilo ni muhimu na la kihistoria si tu kwa kiwanda hicho bali kwa sekta ya viwanda vya kimkakati nchini.


"Nimefarijika kuona muitikio wenu wanakibaha kushuhudia tukio hili kwani Mkataba huu ni mwanzo wa kupiga hatua katika mapinduzi ya kilimo nchini kupitia sekta ya Kiwanda"amesema.


Amesema kuwa uwepo wa kiwanda hicho ni moja ya hatua ya kukuza mahusiano ya kiuchumi na nchi za Cuba na Tanzania jambo ambalo ni la kijvunia.


Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Taifa la Maendeleo nchini (NDC) DK Edwinpaul Mhede amesema kusainiwa kwa Mikataba hiyo kutaleta ahueni ya bei ya mbolea kwa Watanzania okizingatia kuwa asilimia 70 hadi 80 ya wanachi ni wakulima ambapo wamekuwa wakitumia gharama kubwa kununua mbolea.


Naye Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa kimataifa katika Wizara ya Kilimo ya Cuba Orlando Diaz Rodriguez amesema Tanzania na Cuba zimekuwa na mahusiano mazuri zaidi ya miaka 60 iliyopita na kwamba itaendeleza historia hiyo iliyoasisiwa na viongozi waanzikishi wa nchi hizo.


Amesema nchi ya Cuba imekuwa ikiwekewa vikwazo mbalimbali vya kutoka taifa la Marekani lakini imekuwa ikijitahidi kujinasua na hali hiyo hivyo kwa kuendelea na mahusiano mazuri na Tanzania taifa hilo limekuwa linajivunia.


Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC Nicolaus Shombe amesema mikataba hiyo italeta tija kwa nchi hizo mbili kwa nyanja za kiuchumi na kinahusiano zaidi


Mkuu wa Mkoa wa Pwani Abubakari Kunenge amesema Mkoa huo umejidhatiti kuimarisha mazingira bora ya uwekezaji lengo likiwa ni kukuza uchumi wa wananchi na Serikali kwa ujumla.

Share To:

Post A Comment: