Mkuu wa Wilaya ya  Simanjiro Dkt. Suleiman Serera ameipongeza Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela kwa kuleta mapinduzi katika sekta ya elimu ya juu hususani eneo la utafiti na Ubunifu. Dkt. Serera ametoa Pongezi hizo, Agosti 7, 2022 alipotembelea banda la Taasisi  hiyo katika maonesho ya nane nane kanda ya Kaskazini viwanja vya Themi Arusha .


"Wito wangu kwa taasisi  ni kuendelea kuatamia wabunifu tangu wakiwa wadogo ili kuwaendeleza na kupata watafiti wazuri na wabobezi katika kutatua changamoto zinazoikabili"amesema  Dkt. Serera


Alizidi kueleza kuwa, Serikali itazidi kushirikiana na taasisi hiyo   katika kuhakikisha vipaji vya watafiti na wabunifu vinaendelezwa, na kuzidi kuleta chachu ya maendeleo  kwa jamii.


Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya  Nane Nane kutoka Taasisi  hiyo,  Prof. Gabriel  Shirima  ameahidi kufanyia kazi ushauri katika kuboresha eneo hilo la Utafiti  na Ubunifu.


Dkt. Serera alipata fursa ya kuongea  na wananchi waliohudhuria mafunzo ya Kilimo Endelevu  kukabiliana na Mabadiliko ya Tabia ya nchi,  yanayotolewa bure na  taasisi hiyo, na kuwataka wananchi hao kutumia fursa hiyo adimu ili kuboresha kilimo.

Share To:

Post A Comment: