MKUU mpya wa Mkoa wa Tanga, Omary Mgumba amefanyiwa maombi maalum na Viongozi wa Dini zote lengo likiwa ni kumtakia heri na baraka katika majukumu yake mapya ya kumsaidia kazi Rais Samia Suluhu Hassan katika mkoa huo.


Maombi hayo yamefanyika katika Kijiji cha Manga kilichopo Mkata Wilayani Handeni ambapo viongozi kadhaa wa kiserikali wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Siriel Mchembe, Mkurugenzi wa Halmashauri, Saitoti Zellote pamoja na Viongozi wa Chama cha Mapinduzi.


Akizungumza mara baada ya Dua na Maombi hayo, RC Mgumba amewashukuru wananchi wa Handeni kwa mapokezi na maombi hayo ambapo amewasihi kuendelea kufanya kazi ili kuunga mkono juhudi za Rais Samia za kuwaletea maendeleo wananchi wa Tanga na Watanzania kwa ujumla.


" Niwashukuru sana kwa Dua na Maombi haya, naamini kazi inaenda na Sala, niwasihi kufanya kazi kwa bidii ili tukuze Mkoa wetu, lakini pia niwasihi kujitokeza kwa wingi Agosti 23 kushiriki zoezi la Sensa na Makazi," Amesema Mgumba.


Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Siriel Mchembe amemuahidi RC Mgumba kwamba Wilaya ya Handeni wamejipanga kufanya kazi na kutekeleza maelekezo yote ambayo yamekua yakitolewa na Serikali katika kuwahudumia na kuwatumikia wananchi wa Handeni.


" Nikutoe shaka Mhe RC sisi Handeni tumejipanga kuhakikisha tunafanya kazi kwa nguvu na weledi lakini pia kuwatumikia wananchi wetu kwa uadilifu, lengo letu ni kuona azma ya Rais wetu Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea maendeleo inatimia.


Tumejipanga pia kuhakikisha tunahamasisha na kutoa elimu ya Sensa kwa wananchi wetu ili Agosti 23 wajitokeze kwa wingi kuhesabiwa, tumewaeleze kuwa kujitokeza kwao kutasaidia kuiwezesha Serikali kupata Mipango yake ya maendeleo kwa urahisi zaidi," Amesema DC Siriel.


















Share To:

Post A Comment: