Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel (kulia) amekabidhi rasmi ofisi kwa Mkuu mpya wa Mkoa Mwanza, Adam Malima.

Akizungumza kwenye makabidhiano hayo yaliyofanyika Agosti 03, 2022, Mhandisi Gabriel amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumuwezesha kuteuliwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza katika kipindi cha kuanzia Juni 11, 2021 hadi Agosti 01, 2022.

Pia ametumia nafasi hiyo kuwaasa watumishi mkoani kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kutojihusisha na rushwa pamoja na kuendelea kumuombea Rais Samia ili Taifa lizidi kwenda mbele zaidi kimaendeleo.

"Lipendeni Taifa lenu la Tanzania kwani watumishi mmepewa dhamana katika nafasi mbalimbali hivyo mnapaswa kutumia akili zenu na elimu mliyonayo ili kuweza kulitendea haki Taifa, ukiendekeza rushwa unalisaliti Taifa lako" amesema Mhandisi Gabriel.

Kwa upande wake Mkuu mpya wa Mkoa wa Mwanza, Adam Malima ameahidi kushirikiana vyema na watumishi mkoani Mwanza ili kuendeleza utendaji kazi wenye tija kimaendeleo.

Amesema Mwanza ni Mkoa wa kimkakati kiuzalishaji na biashara hivyo atashirikiana na wafanyakazi na wafanyabiashara katika sekta za umma na binafsi ili kupata mawazo yao yatakayokuza maendeleo ya Mkoa.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel (kulia) na Mkuu mpya wa Mkoa Mwanza, Adam Malima wakisaini hati ya makabidhiano ya ofisi.
Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel (kushoto) akiteta jambo na Mkuu mpya wa Mkoa Mwanza, Adam Malima (kulia).
Share To:

Post A Comment: