Leo 06/07/2022 ni maamuzi ya Mahakama kuhusu maombi ya Halima Mdee na wenzake 18 kuiomba Mahakama kufungua Shauri la Msingi ambalo ni kupinga utaratibu uliotumika kuwavua uanachama ndani ya CHADEMA.


Itakumbukwa June 22, 2022 Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam chini ya Jaji Mgeta aliondoa (struck out) maombi ya Wabunge hao 19 ya kufungua Shauri la Msingi kupinga utaratibu uliotumika kuwavua uanachama wao ndani ya CHADEMA kutokana kile kilichoelezwa kuwa maombi yao yalikuwa na kasoro za kisheria.


Kasoro ya msingi iliyotajwa na kuwekewa pingamizi na upande wa CHADEMA ni kuwa maombi hayo yalikuwa yanaishitaki Board of trustee of Chama cha Demokrasia na Maendeleo badala ya Registered trustees of Chama cha Demokrasia na Maendeleo.


Kasoro hizo za kisheria zilizojitokeza hazikuwa za kuwafungia Mlango wa Mahakama Halima Mdee na wenzake 18 kwani bado Sheria iliruhusu kufanyiwa marekebisho na kufunguliwa upya hapo hapo Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam jambo lililofanyika ndani ya muda.


Kuondolewa kwa mapingamizi Mahakamani.


Moja ya jambo lililopelekea kuondolewa kwa mapingamizi ni kwamba kwenye hati ya kiapo kinzani ya upande wa mjibu maombi namba mbili katika kesi No. 27 ya 2022 Kati ya Halima Mdee na wenzake 18 ni kwamba Mawakili wa CHADEMA walijiita Board of trustees of Chama Cha Demokrasia na Maendeleo badala ya Registered trustees of Chama Cha Demokrasia na Maendeleo na jina hilo ndilo lililopelekea kesi kuondolewa Mahakamani hapo awali na Jaji Mgeta.


Hata hivyo Jaji Ismail anayesimamia kesi hiyo hivi sasa hakuamini kosa hilo la jina lina uzito mkubwa hivo ailishauri jina lirekebishwe kwa 'Kalamu' tu na kuruhusu pande zote mbili kukubaliana kuondoa mapingamizi yao.


Kufunguliwa kwa Shauri la msingi kupinga maamuzi ya kufutiwa uanachama kwa Wabunge hao 19.


Hoja za msingi ili maombi ya kufungua mapitio ya kimahakama ( Judicial Review) yakubaliwe ni lazima Mahakama walau ijiridhishe juu ya Mambo yafuatayo:


1. Kwamba waleta maombi wana maslahi kwenye swala lililopelekea kesi kufunguliwa, kwa maana ya kwamba ni waathirika wa jambo hilo lililopelekea kesi kugunguliwa.


2. Kesi iwe imefunguliwa ndani ya miezi sita tangu maamuzi ya mwisho yalipofanyika, na ikumbukwe pia marejeo ya kimahakama hufanyika baada ya kuwa umemaliza nafuu zote ndani ya chama( internal remedies) mfano rufaa ndani ya chama na kwamba hakuna rufaa zaidi kwa mujibu wa mfumo wa ndani ya chama.


3. Kuwe kuna hoja zinazopelekea uwepo wa hoja zenye mashiko na zenazoweza kujenga kesi yenye mashiko (arguable case).


4. Maamuzi yanayopingwa yawe yanatokana na utekelezaji wa jukumu la umma au jukumu ambalo lipo kwa mujibu wa sheria. Mfano suala la kuwapa nafasi ya kujitetea wanachama kabla ya kufukuzwa ni takwa la Katiba ya Tanzania ibara ya 13(6) (a) na kifungu cha 6 (C)(5) ya Sheria ya vyama vya siasa kifungu kinachotaka mwanachama asifukuzwe hadi mifumo yote ya haki (due processes) kwa mujibu wa Katiba ya vyama vya siasa. Hili ni takwa lenye uzito mkubwa kwenye utoaji wa haki.


5. Kusiwe kuna afueni nyingine nzuri zaidi ya marejeo ya kimahakama (no other adequate and convenient remedy).


Je hoja hizo 5 Halima Mdee na wenzake 18 wamekidhi vigezo vya kufungua shauri la Msingi? Hili ni swali tunaloliachia Mahakama Kuu Kanda ya Dar es salaam kutupatia majibu leo hii.

Share To:

Post A Comment: