Wizara ya Afya imepokea vifaa tiba vya matibabu ya macho vyenye thamani ya shilingi milioni 110 kutoka Shirika la Helen Keller International kupitia mradi wake wa CAMBI Project unaotekelezwa katika wilaya ya Mbarari mkoani Mbeya.


Akizungumza katika makabidhiano ya vifaa hivyo yaliyofanyika jijini Mbeya, Meneja wa Mpango wa Taifa wa huduma za macho Wizara ya Afya Dkt. Benadertha Shillio amelishukuru Shirika la Helen Keller International na amesema kuwa uwepo wa vifaa tiba hivyo utawanufaisha wananchi kwenye huduma za matibabu ya mtoto wa jicho zitakazotolewa katika hospitali ya wilaya ya Mbarari kwa kushirikiana na wataalamu kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya, hivyo kutawaepushia wananchi gharama ya kufuata umbali mrefu.


Akitoa takwimu za ugonjwa huo duniani Dkt. Benadertha amesema katika kila mtu mmoja kati ya 100 ana ulemavu wa kutokuona kabisa na inakadiriwa watu wanne kati ya watu 10 wana upungufu wa kuona wa kati na ule wa juu, na watu 20 kati ya watu 100 wana tatizo linalohusiana na macho.


Naye Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji amesema matatizo ya macho kwa wakazi wa nyanda za juu kusini ni makubwa, hivyo ujio wa mradi huu utasaidia kufanikisha matibabu ya wananchi wa mkoa wa Mbeya na wilaya ya Mbarari na kufanya huduma za matibabu ya mtoto jicho kuwa endelevu.


Kwa upande wake mwakilishi wa Helen Keller International Tanzania, Ndg. Deogratias Ngoma ameishukuru Serikali na Wizara ya Afya kuwa ushirikiano na kwa kuupokea mradi huo wa CAMBI Project ambao ni wa kipekee na wanatarajia kwa muda wa mwaka mmoja na nusu wananchi zaidi ya  900 wa wilaya ya Mbarari watapatiwa matibabu ya upasuaji ya mtoto wa jicho na kueleza kuwa kupitia mradi huo wataalamu wa macho watapita nyumba kwa nyumba katika ngazi ya kitongoji kutoa elimu na watakaoonekana na ugonjwa wa mtoto wa jicho wataenda hospitali kupatiwa matibabu.


Naye Patricia Mwalusi, Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mbarari amelishukuru shirika la Helen Keller International kwa kuleta mraji huo wa matibabu ya mtoto wa jicho ambao una manufaa kwa wananchi wa wilaya ya Mbarari na vitongoji vyake.

Share To:

Post A Comment: