NA OR-TAMISEMI


WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Mhe. Innocent Bashungwa amekerwa na hali ya uzembe ya kutokamilishwa kwa mradi wa ujenzi na ukarabati wa majengo katika Chuo cha Ufundi VETA-Karagwe (KDVTC) zaidi ya miaka minne mpaka sasa, tangu Oktoba 2018.


Bashungwa ametoa kauli hiyo leo Juni 12, 2022 baada ya kukagua majengo na kusomewa taarifa hali iliyomfanya kutokuridhishwa na namna Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) anavyotekeleza mradi wa ujenzi wa Chuo cha Ufundi VETA Karagwe (KDVTC) kwa gharama ya shikingi bilioni 4.65.


“Tangu Oktoba 2018 mkandarasi alipokabidhiwa mradi na ukifuatilia mchakato tangu wakati huo mpaka sasa hivi, inaonesha hakuna mwenye haraka upande wa TBA vile vile upande wa VETA, wakati mitambo na zana za kufundishia tayari zimeshanunuliwa,”amesema Bashungwa.


Bashungwa amesema, ndani ya muda mfupi watakutana kwa pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda kwa upande na VETA na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa upande wa TBA ili kupata mwarobaini wa uzembe na ucheleweshwaji wa kukamilika kwa mradi huo.


Aidha, Bashungwa ameeleza pamoja na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na viongozi mbalimbali waliotembela na kukagua ujenzi wa chuo hicho, mpaka sasa utekelezaji unadorora mwingine haujafanyiwa kazi kutokana na hali ya uzembe na kufanya kazi kwa mazoea.


Amesema, chuo kikikamilika kitatoa fursa kwa vijana wa Wilaya ya Karagwe na wilaya jirani kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi yatakayokuza uchumi binafsi na Taifa kwa ujumla na kusaidia upatikana wa wataalam wataotumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.


Mradi  huo wa Chuo cha VETA Karagwe unahusisha ujenzi wa jengo la utawala, madarasa, choo cha madarsa, stoo, bwalo la chakula, karakana ya umeme, jengo la mafunzo mbalimbali, choo cha wasichana, bweni la wavulana na ukarabati wa karakana ya uchomeleaji, karakana ya magari na karakana ya ushonaji.

Share To:

Post A Comment: