Na Mathias Canal, WEST-Dodoma


Serikali imekusudia kuimarisha ubora wa elimu nchini ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa inaakisi mahitaji ya watanzania na utandawazi na kasi ya mabadiliko ya teknolojia kwani soko la ajira limezidi kuwa pana hivyo mabadiliko yanahitajika.


Utandawazi huo ni pamoja na watanzania kuchukua fursa ya kufundisha lugha kiswahili katika vyuo kwenye nchi mbalimbali Duniani.


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof. Adolf Mkenda ameyasema hayo tarehe 9 Juni 2022 wakati wa kikao kazi cha Tathmini ya utendaji kazi idara ya uthibiti ubora wa shule kati ya viongozi, uthibiti ubora wa shule na makao makuu, ithibati ya shule na wathibiti ubora wa shule wakuu kanda na wilaya iliyofanyika katika ukumbi wa vijana Jijini Dodoma.


Amewataka wathibiti ubora kote nchini kusimamia kwa weledi zaidi ubora wa elimu kwani wao ni moyo na injini ya elimu.


Amesisitiza umuhimu wa malezi kwenye shule kwani watoto wanaanza shule mapema huku wazazi wakiwa kwenye kinyang'anyiro cha maisha hivyo watoto wanakuwa katika mazingira ambayo hayaakisi afanisi na nidhamu bora kwa mtoto.


"Tunaona kwenye mitandao mambo ya hovyo yanatokea na sisi tusingependa kupuuza tutakuja na tamko na mikakati baada ya kupitia" Amekaririwa Waziri Mkenda na kuongeza kuwa 


"Nyie ni mboni ya elimu hapa nchini, mnapaswa kutunzwa, kuheshimiwa na kulindwa ili elimu iweze kuwa bora, hivyo pambaneni serikali imewanunuliwa magari 74 na mambo mengine chungu nzima yanakuja, msichoke"


Waziri Mkenda amesema kuwa Uboreshaji wa elimu kwa kupitia sera ya elimu ya mwaka 2014 na mapitio ya mitaala sio ajenda ya mtu, hiyo ni agenda ya serikali ya Tanzania inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo maagizo hayo aliyatoa wakati akihutubia Bunge la 12 tarehe 22 Aprili 2021 Jijini Dodoma.


Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknoloji Prof James Mdoe amempongeza Waziri Mkenda kwa kuwathamini wathibiti ubora kwa kutenga muda kuhudhuria katika mkutano huo kwani amewaongezea nguvu na ufanisi wa kazi.


Amesema kuwa bila elimu msingi iliyo bora ngazi zingine zote zitakuwa ngumu katika kuthibiti ubora ipasavyo hivyo amewasihi kuongeza weledi kwa ajili ya kazi hiyo.


"Kuna zoezi muhimu sana linaendelea la kupitia mitaala na sera ya elimu na mafunzo hivyo wathibiti ubora wanapaswa kushiriki kwa kina katika zoezi hilo kw kiwango kikubwa kwani haitakuwa na maana kama msiposhiriki" Amekaririwa Prof Mdoe


MWISHO

Share To:

Post A Comment: