Wadau wa Kilimo wametakiwa kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza kwenye miundombinu ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.


Akizungumza wakati ufunguzi wa Kongamano la Nane la Mwaka la Wadau wa Sekta ya Mazao, Mifugo na Uvuvi, Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe amesema ni wakati wa wadau kutumia vizuri utayari wa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuikuza sekta ya Kilimo na kuondoa umasikini kwa wakulima.

Aidha Mhe. Bashe ameitaka sekta binafsi na Wadau wa Maendeleo kwenye Kilimo kuelekeza fedha kwenye miundombinu ya umwagiliaji na uhifadhi.

"Hawa wakulima wanaomiliki mashamba madogo hawana uwezo wa kuwekeza kwenye miundombinu ya umwagiliaji au maghala ya kuhifadhi mazao,ni vema rasilimali zilizopo zikaelekezwa katika maeneo hayo". Amesema Mhe. Bashe.

Mhe. Bashe amefafanua kuwa endapo mkulima atawezeshwa kwenye miundombinu ya umwagiliaji na uhifadhi itamsaidia kulima kulima kwa uhakika na kumuepusha na upotevu wa mazao baada ya kuvuna ambao hutokea wakati wa kuvuna, kusafirisha na kuhifadhi.

Mhe. Bashe amekumbusha kuwa biashara kubwa Duniani itakuwa chakula lakini atakayenufaika na biashara hiyo ni yule aliyejiandaa na tayari Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha nia ya kuwaweka Watanzania kuwa tayari na biashara ya kilimo.

Awali akimkaribisha Waziri Bashe, Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Hamis Hamza Hamis amesema athari za mabadiliko ya tabia nchi zimeshajitokeza kwenye sekta nyingi zikiwemo kilimo, mifugo na uvuvi hivyo lazima hatua zichukuliwe kulinda rasilimali zinazotunza mazingira.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Kilimo Tanzania Bi. Jacquline Mkindi ametoa pongezi kwa Waziri Bashe kwa kuwa na maono ya kujumuisha vijana kwenye sekta ya Kilimo.


Share To:

Post A Comment: