Mkuu wa Mkoa wa Arusha John Mongella amesema hakuna Mwananchi yoyote ambaye yako kwenye tarafa ya Ngorongoro ambaye amelazimishwa au kushurutishwa kuhama bali wote wanaohama kwenda Msomela wilayani Handeni wameamua kwa hiyo.


Akizungumza mbele ya waandishi wa habari wakati wa kushuhudia wananchi walioamua kuhama kwa hiyari Ngorongoro ikiwa ni kuitikia mwito wa Serikali Mongella amesema hakuna mtu yoyote aliyeshurutishwa kuhama.

"Hakuna mtu ameshurutishwa wala kulazimishwa na mmeona baada ya wengine hawa kutoka kule Msomela wilayani Handeni sasa hivi kuna wimbi kubwa la wananchi wanaotaka kwenda kule ambako Serikali kwa upendo wake mkubwa imeweka miundombinu yote muhimu ya huduma za kijamii.

"Naomba ichukue fursa hii kusema, hapa kuna mkanganyiko kidogo ambao ningependa kutoa ufafanuzi, wilaya ya ngorongoro ina tarafa tatu ,tarafa ya Ngorongoro hii tuliopo , tarafa ya Loliondo na tarafa ya Sare . kutoka tarafa ya makao makuu ya Ngorongoro kufika Loliondo ni takriban saa nne hivi .

"Kufika tarafa ya Sare ni takriban saa tatu na nusu au nne, kwa hiyo naomba watu waelewe tarafa ya Ngorongoro na tarafa ya Loliondo ni vitu viwili tofauti .Ajenda ya Ngorongoro ni kuimarisha uhifadhi ambapo tuna tunu hizi kubwa tulizojaaliwa na Mungu kama urithi wa dunia,"amesema Mongella.

Amefafanua ukweli ni kwamba idadi ya mifugo na watu inaongezeka kulinganisha na mwaka 1959 ambako hifadhi hiyo ilitangazwa kisheria pamoja na kufanyika maboresho mengine ya kisheria.

Amesema kinachofanyika Ngorongoro ni wale ambao kwa hiyari yao wako tayari kuhamia Msomela eneo ambalo limetengwa na Serikali , ambalo lina rutuba , eneo la malisho na huduma za kijamii zilizowekezwa na Serikali na hawa waliojitokeza kwa uzalendo kabisa waende kule wakafanye maisha bora zaidi.

"Mtakumbuka hapa Ngorongoro kwa mujibu wa sheria mtu haruhusiwi kumiliki ardhi, mtu hawezi kujenga makazi ya kudumu.Huduma maaboresho yake ni magumu kisheria kwasababu ya uhifadhi, kwa hiyo kimsingi ndugu zetu tukiri kuna maendeleo mengi wameyakosa na kwa muda mrefu imekuwa vigumu wao kujiletea maendeleo hata yao binafsi

"Serikali ya Awamu ya sita imetoa fursa hiyo bila shuruti bila kulazimishwa , hawa wote mnawaona ndio maana sisi serikali ya mkoa tukishirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii na mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro wananchi wenyewe waliojiandikisha tumewaambia hatutagusa majengo yao wala mali zao.

"Mmewaona wanabomoa wenyewe pamoja na fidia ambazo wamepata mali ambazo wanataka kuzibeba wazichukue na tutawapa usafiri bure hadi Msomela wilayani Handeni.Mmmewasikiawenyewe wakitoa ushuhuda na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan,"amesema.

Hivyo amewaomba wale ambao hawaelewi ajenda ya Ngorongoro ndio hiyo aliyoieleza , haina shurutisho lolote, haina lazima yoyote.

"Ajenda kubwa hapa ni uzalendo kulinda maslahi mapana ya dunia na kulinda urithi wa dunia, maslahi mapana ya nchi yetu .Sasa tumeona kwenye mitandao upotoshaji mkubwa unaondelea wa makusudi na mwingine wa kutokujua tu, mtu hajui kitu anataka kuelezea hatari sana hiyo"amesema Mongella.

Ametumia nafasi hiyo kutoa onyo kwa wale wote ambao wameendelea kupotosha nia njema ya Serikali huku akieleza wataokabainika watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria za nchi.

Share To:

Post A Comment: