KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2022,Sahili Geraruma amewataka viongozi kusimamia na kufuatilia miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali.

Kauli hiyo ameitoa wakati mwenge huo ukiwa wilayani Karatu mkoani Arusha kuzindua, kutembelea na kuweka mawe ya msingi katika baadhi ya miradi.

Bw. Geraruma alisema kuwa, kumekuwa na tabia iliyozoeleka kwa baadhi ya viongozi wa Serikali hasa idara ya manunuzi kwa kuidhinisha fedha kwa ajili ya miradi bila ufuatiliaji ili kujua matumizi halali ya fedha zilizoidhinishwa jambo ambalo husababisha miradi mingi kuwa chini ya kiwango.

Alisema kuwa, ni jukumu la wataalamu kutembelea miradi mara kwa mara ili kujua ubora wake na kuweza kurekebisha kabla mradi haujafia mbali kuepuka miradi isiyo na tija.

Kiongozi huyo wa mbio za mwenge aliwataka madiwani pamoja na uongozi mzima wa wilaya kuipa vipaumbele miradi inayoibuliwa na wananchi kwa kutoa michango ili kuwapa moyo wananchi kuchangia miradi.

"Wananchi wanachanga michango wanaanza utekelezaji wa mradi,lakini halmashauri mnakaa muda mrefu kuweka mchango wa halmashauri,"alisema kiongozi huyo.

Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Dadi Kolimba alisema kuwa Mwenge wa Uhuru wilayani Karatu umeweza kuzindua,kufungua na kuweka mawe ya miradi nane yenye thamani ya shilingi bilioni 3.6 ikiwemo michango ya Serikali Kuu,halmashauri ya wilaya pamoja na nguvu za wananchi.

Alifafanua kuwa, kati ya miradi hiyo miradi miwili ilifunguliwa,mitatu ilizinduliwa na miwili ilitembelewa ambapo mradi moja ulitolewa maelekezo.
Share To:

Post A Comment: