WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wafanyabiashara ndogondogo na wajasiriamali wafanye biashara zao kwa uhakika kwa sababu Serikali inataka watimize matananio yao. 

 

“Serikali hii inawatambua na itasimamia matamanio yenu na mtafuika kwenye ndoto zenu. Mtaji uliowekezwa kwenye vibanda hivi na Jiji ni shilingi bilioni moja na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan akaongeza shilingi milioni 500 ili masoko mengi yajengwe,” amesema.

 

Waziri Mkuu ambaye yuko mkoani Arusha kwa ziara ya siku moja, amekagua masoko ya Mbauda, Kilombero na Machame na kuzungumza na baadhi ya wamachinga wanaofanya biashara kwenye masoko hayo.

 

Akizungumza kwa nyakati tofauti na wajasiriamali hao baada ya kukagua kila soko leo (Jumanne, Mei 24, 2022), Waziri Mkuu amesema lengo la Serikali ya awamu ya sita ni kuwawezesha wajasiriamali wadogo wakue kimitaji na kumiliki biashara kubwa.

 

"Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan nia yake ni kuwafanya muweze kuwa na maeneo yanayotambulika, kisha mpate kipato rasmi ili nanyi muwe wafanyabiashara wakubwa hapo baadaye. Hapa Arusha wako wafanyabiashara maarufu ambao walianza kwa kusafisha viatu lakini leo wanamiliki biashara kubwa kubwa," amesema.

 

Amewataka wafanyabiashara hao wahakikishe kuwa wanafanya biashara kwenye maeneo yanayotambulika ili waweze kupatikana kwa urahisi na waweze kupata mikopo ya mitaji kama ambavyo Mheshimiwa Rais alielekeza.

 

"Suala la mitaji, Mheshimiwa Rais Samia alishakutana na wakuu wa mabenki nchini na kuwaomba waweke vigezo ambavyo vitasaidia wajasiriamali wadogo kukopesheka. Ili ukopesheke, ni lazima uwe na anuani, ukiwa na anuani ni rahisi kufuatiliwa unaendeleaje na biashara yako,  mtaji wako ni kiasi gani na pia kupima uwezo wako wa kurejesha endapo utapata huo mkopo."

 

“Niwasihi ndugu zangu wafanyabiashara, fanyeni biashara zenu kwenye meza zinazojengwa kwenye haya masoko. Hiyo meza hapo sokoni ndiyo anuani yako. Uongozi wa soko utajua uko wapi, unauza nini, vina thamani gani. Pia utakudhamini kwa sababu unajulikana unafanyia wapi biashara yako.”

 

“Nendeni kwenye masoko mpate fursa muhimu. Ukikopa, unatakiwa urejeshe ili mwenzio naye apate na pia ukimaliza uweze kukopa kiwango cha juu zaidi. Kopeni na kurejesha ili kukuza mitaji yenu, hatimaye mtakuwa wafanyabiashara wakubwa,”  amesisitiza. 

 

Mapema leo, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa masoko matatu jijini Arusha na kubaini mapungufu kadhaa ikiwemo ukosefu wa maji, umeme, uhaba wa vyoo na bugudha za askari mgambo.

 

Amemwagiza Mkuu wa Mkoa huo, Bw. John Mongella na Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Bw. Said Mtanda wasimamie masuala hayo na kuhakikisha kero hizo zinaondolewa kwa wafanyabiashara hao.

 

"Hapa soko la Kilombero nguzo ya umeme iko nje tu, ni kwa nini inachukua mwezi na zaidi kushughulikia ombi la kuweka umeme wakati barua iliandikwa tangu mwezi uliopita? Hiyo shilingi 500 wanayochangishwa, si bora waitumie kununua luku?

 

Mkazi wa Mbauda, Bi Mary Mushi ambaye ni mfanyabiashara ya nyanya katika soko hilo, alimweleza Waziri Mkuu kwamba wanachangishwa sh. 500 ili kununua dizeli ya kuendesha jenereta linalotumika kutoa umeme sokoni hapo. Umeme huo unawashwa hadi saa 3.30 usiku.

 

Hata hivyo, Waziri Mkuu alipomtaka Meneja wa TANESCO wa wilaya, Bw. Amiri Chambua aseme ni lini wataweka umeme, Bw. Chambua aliahidi kukamilisha kazi hiyo kesho (Jumatano, Mei 25, 2022). Alikiri kupokea barua ya maombi tangu mwezi uliopita na kudai kwamba walikuwa kwenye mchakato wa maandalizi.

 

Kuhusu kadhaa ya askari mgambo, Waziri Mkuu amewataka watumie weledi na maarifa kwenye kazi yao ya ulinzi. “Mtu kama anauza eneo lililoruhusiwa, askari tumieni miongozo na waeleweshwe; na pia zile mali mlizoweka kule Depot warudishieni kwa sababu mitaji ni midogo,” alisema na kuamsha shangwe miongoni mwa wafanyabiashara hao.


 





 

Share To:

Post A Comment: