Na WAF - Kigoma 


Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi ameshauri kuondolewa kwa Mganga Mkuu wa  Wilaya Kigoma kutokana na kushindwa kutekeleza maagizo ya kuboresha huduma, kukosa Uwajibikaji ikiwemo kushindwa kutengeneza boti kwa gharama milioni  moja (1) iliyokuwa ikibeba wagonjwa  na wajawazito katika eneo lake. 


Aidha, Daktari huyo pia alionyesha utovu wa nidhamu wa kushindwa kuhudhuria kikao hicho na hakutoa taarifa Kwa Mganga Mkuu wa Mkoa .


Prof. Makubi ametoa agizo hilo wakati akiongea na Watoa huduma za Afya wa Mkoa wa Kigoma walioongozwa na Mganga Mkuu wa Mkoa huo katika ukumbi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kigoma. 


Amesema, Wapo baadhi ya Waganga Wakuu wa Halmashauri hawawajibiki ipasavyo katika maeneo yao, wengine hawataki kutekeleza maagizo ya viongozi yenye lengo la kuboresha huduma za afya nchini, hawa wanaturudisha nyuma. 


"Miezi mitatu iliyopita Mganga Mkuu wa Serikali alitoa maelekezo ya kutengeneza boti hiyo iliyosaidia sana kubeba wagonjwa wa dharura, pamoja na wajawazito, gharama za matengenezo ya boti hiyo ni milioni moja tu, bado mtu hutekelezi, huyu hafai kuwa kiongozi." Amesema 


Sambamba na hilo Prof. Makubi amewaagiza Waganga Wakuu wa Halmashauri kuwa wazalendo na wawajibikaji ili kuongeza kasi na ufanisi katika kuboresha huduma kwa wananchi hali itakayosaidia kupunguza malalamiko yanayoweza kuzuilika. 


Aidha, Prof. Makubi amesema,  kwa kiasi kikubwa Serikali imeboresha miundombinu katika maeneo ya kutolea huduma za afya, hivyo mkakati wa Wizara kwa sasa ni kusimamia ubora wa huduma ili wananchi wanufaike na huduma hizo katika ngazi zote kuanzia Zahanati mpaka hospitali maalum na Taifa. 


Hata hivyo, Prof. Makubi amewaelekeza Waganga Wakuu wa Halmashauri kusimamia hali ya dawa katika maeneo yao, ili kuondokana na changamoto ya upungufu au upotevu wowote wa dawa ili wananchi wasikose huduma hiyo. 


Mbali na hayo, amewaelekeza kuanzisha vigoda vya huduma kwa mteja kwa ambao bado hawajaanzisha, kwani itasaidia kusikiliza malalamiko, kero, maoni au pongezi juu ya huduma wanazotoa ili kuboresha zaidi. 


Pia, Prof. Makubi ameelekeza kuhakikisha wanafunga mifumo katika vituo vyao ili kuondoa changamoto ya upotevu wa mapato na dawa katika maeneo yao, hali itayosaidia katika kuboresha huduma katika maeneo yao. 


Sambamba na hilo amewataka kuendelea kutoa Elimu kwa jamii juu ya magonjwa yasiyoambukiza, kwani tatizo hilo limeendelea kuongezeka kwa kasi nchini na kuongezea mzigo Serikali katika matibabu yake, pesa ambayo ingeweza kutumika katika maeneo mengine ya uboreshaji wa huduma. 


Prof. Makubi amewataka kufufua kamati za afya za vijijini ambapo ndio changamoto za wananchi hupatikana, huku akisisitiza kufanya hivyo kuwasaidia kutatua changamoto nyingi ikiwemo suala la vifo vya mama na mtoto kwa kutoa elimu kwa wananchi. 


Share To:

Post A Comment: