Na Ahmed Mahmoud 

Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Francis Michael amezinduwa rasmi kamati ya Kitaifa ya maandalizi ya mkutano wa Shirika la Utalii Duniani Kamisheni ya Afrika ( 65th UNWTO-CAF MEETING) utakaofanyika Jijini Arusha tarehe 5 – 7 Oktoba, 2022. Mkutano huu wa 65 unakauli mbiu  isemayo ‘’Rebuild Africa Tourism Resilian for Africa” unatarajiwa kuhudhuriwa na Mawaziri wenye dhamana ya sekta ya Utalii na Uhifadhi kutoka katika nchi wanachama wa UNWTO.

“Nategemea kamati hii itafanya kazi kwa weredi, maarifa na kuwa na kasi kubwa katika maandalizi haya. Nipo tayari kushirikiana nanyi muda wowote kwani lazima tuhakikishe kuwa Tanzania inakuwa mfano kwa nchi nyingine wananchama wa umoja huu.  Nina nafasi ya kufanya mabadiliko ya wajumbe wakati wowote pale ninapoona maandalizi yanalegalega”, aliyasema hayo Dkt. Francis wakatika wa uzinduzi wa Kamati uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Ngorongoro Crater uliopo katika jengo la Kituo cha Utalii Ngorongoro jijini Arusha. 

Kamati ya Maandalizi ya Kitaifa ambayo itakuwa na wenyeviti Wenza wawili ambao ni Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Bw. Felix John na mwenyekiti mwenza Bw. Rahim Bhaloo ambaye ni Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, wataongoza kamati ya wajumbe kutoka kwenye baadhi ya Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Maliaisili na Utalii, Taasisi na Idara za Wizara mbalimbali, vyama vya wadau wa utalii na waandishi habari wa Tanzania.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Tanzania, Felix John amesema, “Mkutano wa 65 wa UNWTO kufanyika Tanzania ni sehemu ya utekelezaji wa vitendo wa mkakati wa Bodi ya Utalii wa kutangaza na kukuza utalii wa Mikutano (MICE) ambao unalenga kuvutia mikutano mingi ya kimataifa kufanyika nchini Tanzania. Wito wangu kwa wadau wa utalii, wajitayarishe kutoa huduma nzuri kwa ugeni huu ili tuendelee kuiweka nchi ya Tanzania kwenye nafasi nzuri ya kuaminiwa kuandaa mikutano mingine ya kimataifa.


Naye Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar (ZCT), Rahim Bhalloo alieleza kuwa, Mkutano huu ni fursa kwa nchi ya Tanzania kuuza mazao ya utalii na uwekezaji katika sekta ya utalii. Vilevile ni fursa kwa wananchi wa Tanzania kuwa wabunifu ili waweze kufanya biashara na kujiongezea kipato kupitia mkutano huo wa 65 wa UNWTO-CAF.Share To:

Arusha Newsroom

Post A Comment: