Jeshi la Polisi mkoani Mara linamshikilia mtu mmoja ambaye jina lake halijajulikana kwa kosa la kupanda juu ya nguzo ya umeme, huku lengo lake likiwa bado halijajulikana.


Mkuu wa Wilaya ya Butiama, Moses Kaegele amesema kuwa mtu huyo alipanda kwenye nguzo ya umeme iliyopo katika Kijiji cha Mwibagi kando ya Barbara ya Musoma- Mwanza ambapo hadi sasa bado haijajulikana alikuwa na lengo gani.

Amesema kuwa baada ya tukio hilo watumishi wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Mkoa wa Mara walifika katika eneo hilo na kumshusha mtu huyo kisha kumkabidhi kwa polisi kwa ajili ya mahojiano zaidi.


"Ni kweli kuna hilo tukio lilitokea jana jioni lakini taarifa zaidi nitatoa baada ya kupata ufafanuzi kutoka polisi ambao hivi sasa wanaendelea na mahojiano kwa hiyo naomba uwe na subira" amesema Kaegele.

Naye Meneja wa Tanesco Mkoa wa Mara, Hussein Mwankunja amesema taarifa zaidi ya tukio hilo atazitoa baadaye.

"Kuna fundi ambaye alikuwa eneo la tukio tusubiri aje na taarifa yenye ufafanuzi zaidi ili niweze kuwapa," amesema.

Kamanda wa Jeshi la Uokoaji na Zimamoto Mkoa wa Mara, Agostino Magere amesema kuwa bado ofisi yake haijapata taarifa zaidi ingawa taarifa za awali ni kwamba mtu huyo hivi sasa anahojiwa na jeshi la polisi.

"Jana Tanesco walilazimika kukata umeme ili kumshusha mtu huyo na walifanikiwa, baada ya hapo alikabidhiwa polisi kwa ajili ya mahojiano, hadi sasa sina taarifa huyu mtu anaitwa nani, umri wake, makazi yake na lengo la kupanda kule juu hebu tusubiri polisi watabaini nini," amesema.

Kaimu Kamanda wa polisi Mkoa wa Mara aliyetambuliwa kwa jina moja la Mapuli hakupatikana kuzungumzia suala hilo baada ya simu yake kuita bila kupokelewa.

Share To:

Adery Masta

Post A Comment: