Na,Moses Mashalla,Arusha


Zaidi ya wakazi 40 Mkoani Arusha wamemuomba waziri wa ardhi ,nyumba na maendeleo ya makazi ,Angeline Mabula kuingilia kati mgogoro wa ardhi baina yao na halmashauri ya Arusha uliodumu kwa takribani zaidi ya miaka mitano mpaka sasa.


Wakazi hao wamemuomba waziri Mabula kuingilia madai yao baada ya kulalamika kwamba wameshindwa kuendeleza makazi yao kwa zaidi ya miaka mitano kufuatia halmashauri ya Arusha kushindwa kuwamilikisha ardhi kisheria kwasababu ambazo hazijawekwa wazi mpaka sasa.


Mmoja wa wakazi hao,William Ernest alisema kwamba mwaka 2018 alinunua kiwanja kutoka kampuni ya Ardhi Plan Ltd katika eneo la Mlangarini na mwishoni mwa mwaka jana alipotaka kuendeleza kiwanja chake aliletewa barua ya kusitisha ujenzi kwa kuwa hakuwa na kibali cha ujenzi.


"Niliambiwa kwamba sina kibali cha ujenzi na baada ya kufuatilia kibali halmashauri hakuna majibu sahihi ninayopewa mpaka leo " alisema Ernest


Hatahivyo,Ernest alimuomba waziri Mabula kuingilia kati suala hilo kwa kuwa ametumia gharama nyingi kununua kiwanja hicho na mpaka sasa ameshindwa kukiendeleza kwasababu ambazo hazieleweki.


Sabina Francis,alisema kwamba alinunua kihalali kiwanja mwaka 2018 katika eneo la Mlangarini na kupatiwa mkataba na kampuni ya Ardhi Plan Ltd lakini mpaka sasa ameshindwa kuendeleza kutokana na kushindwa kumilikishwa na halmashauri ya Arusha.


Alisema kwamba pamoja na kufanya jitihada za kufika katika ofisi za ardhi katika halmashauri ya Arusha na kutuma maombi ya kumilikishwa kisheria eneo hilo lakini mpaka leo hajapatiwa majibu sahihi na kumuomba waziri Mabula kuingilia kati.


"Mimi nilinunua eneo langu kihalali mwaka 2018 na kupewa mkataba kabisa lakini ghafla nilipotaka tu kuendeleza nikalatewa barua ya kusimamisha ujenzi naomba waziri atusaidie" alisema Sabina


Naye,Japhet Langoi alisema kwamba baada ya kununua eneo mwaka 2019 alituma maombi ya kupatiwa hatimiliki mbele ya halmashauri ya Arusha lakini mpaka leo anashangaa ni kwanini hajapatiwa hatimiliki na wala kupewa majibu kwa maandishi nini kimeshindikana.


Mkurugenzi wa halmashauri ya Arusha,Seleman Msumi alipotafutwa kuzungumzia madai hayo alisema kwa kifupi eneo hilo lina mgogoro kwa kuwa kuna viwanja vimeuzwa kwa zaidi ya mtu mmoja na kuwataka wenye malalamiko wayafikishe mahakamani.



Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Ardhi Plan Ltd ambayo imeuza viwanja katika eneo hilo,Gombo Simandito alipoulizwa alisema kwamba kampuni yake haijauza viwanja kwa zaidi ya mtu mmoja katika eneo hilo na haelewi kwanini halmashauri inashindwa kuwamilikisha ardhi kisheria wananchi hao kwani baadhi yao tayari wameshamilikishwa na kupatiwa hatimiliki.


Hatahivyo,uchunguzi wa blog hii umebaini ya kwamba katika eneo la Mlangarini baadhi ya watu tayari wameshamilikishwa kisheria maeneo hayo huku wengine wakiwa bado mpaka sasa.


Uchunguzi huo umeenda mbali zaidi na kubaini ya kwamba baadhi ya watumishi wa idara ya ardhi katika halmashauri ya Arusha wanamiliki viwanja katika eneo hilo na baadhi yao wamekuwa wakiomba kupewa rushwa ili kuwamikilikisha baadhi ya watu wenye viwanja katika eneo hilo.


Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa mmoja wa maofisa wa idara ya ardhi katika halmashauri hiyo (jina limehifadhiwa) amekuwa akikwamisha zoezi la baadhi ya wakazi hao kumilikishwa ardhi kutokana na kuwa na mgogoro wa kimaslahi na kampuni ya Ardhi Plan iliyouza viwanja hivyo .


Mwisho.

Share To:

JUSLINE

Post A Comment: