Serikali mkoani Arusha imewataka wadau wa mazingira mkoani hapo kuachana na dhana ya kutoa fedha katika kipindi za maadhimisho ya upandaji miti badala yake watoe rasilimali hiyo kwa ajili ya urithi wa vizazi vijavyo.
Akizungumza katika kilele cha upandaji wa miti uliofanyikia kitongoji cha Mringa wilayani Arumeru mkoani humo ambapo kauli mbiu ni mti wangu,Taifa langu,mazingira yangu na kazi iendelee, Mkuu wa mkoa wa Arusha,John Mongella alisema ni vyema wadau hao wakatoa miche kuliko fedha ili viongozi kuanzia ngazi ya mtaa wahusike katika vitendo katika upandaji wa miti."Kuanzia leo programu yetu ni kukusanya miti na hiyo ndio kampeni nitakayoiongoza na ninaanzisha timu maalumu ya kukusanya miche natusipoweka bidii vizazi vijavyo vitateseka kwa uzembe wetu,"alisema Mongella.Mongella alisema mkoa wa Arusha unayo maeneo ya kuotesha miti kirahisi hivyo maelekezo yake kwa wakuu wa wilaya na wakurugenzi waanze programu ya upandaji wa miti kuanzaia leo Aprili 8,2022 ili kuweza kubadilisha mazingira ya maeneo yenye ukame.
Afisa maliasili Mkoa wa Arusha,Julius Achiula alisema wanaendelea kuelimisha na kuikumbusha jamii juu ya umuhimu wa upandaji miti ili kuweza kufaidia na mazao pamoja na huduma zipatikanazo kutoka kwenye miti na misitu ambayo imehifadhiwa kupitia ushirikiano wa pamoja."Mkoa unaendelea kuratibu na kusimamia utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya upandaji na utunzaji miti inayoelekeza kila halmashauri ya wilaya kutenga maeneo na kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka,"alisema Afisa maliasili huyo.Achiula alisema katika utekelezaji wake kwa vitendao halamashauri zote mkoani Arusha zimekuwa na desturi za upandaji wa miti ingawa hazikuweza kufikia lengo la serikali la kupanda miti milioni 1.5 kwa kila halmashauri kwa mwaka tangua agizo hilo lilipoasisiwa mwaka 2009.Alisema changamoto zilizokwamisha lengo hilo ni pamoja na uwepo wa ukame wa muda mrefu katika maeneo mengi hali iliyosababishwa na mabadiliko ya tabia ya nchi ,uharibifu wa miti kutokana na uwepo wa mifugo pamoja na uhaba wa upatikanaji wa miti ya kupandwa hususani katika maeneo ya mijini.Aidha alisema kuwa katika msimu wa mwaka 2020/2021 idadi ya miti iliyopandwa ni milioni 2,68,840 na iliyostawi ni milioni 1,66,384 sawa na asilimia 78 ikiwa takwimu hizo zinahusisha miti yote iliyopandwa na halmashauri za wilaya pamoja na jiji,Taasisi za serikali,Asasi za kiraia ,vikundi vya mazingira na watu binafsi.Afisa huyo alisema zoezi la upandaji wa miti hufanyika mara nyingi katika msimu wa mvua,pamoja na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi bado wameweka mkazo mkubwa katika upandaji wa miti ya matunda katika maeneo ya shule ili kuchangia lishe kwa wanafunzi hali itakayosaidia kuondolea  magonjwa ya kwashakoo kwa baadhi ya wanafunzi katika shule mbalimbali mkoani hapo.

Share To:

Post A Comment: