Teddy Kilanga, Arusha

Kutokana na changamoto ya baadhi ya wananchi kutokuelewa umuhimu wa mahakama na kazi zake,Mahakama ya rufani ya Tanzania imezindua jarida ambalo litasaidia kutoa elimu kwa wananchi na wadau mbalimbali ili kuweza kupata uelewa wa utendaji wa mahakama hiyo nchini.



Akizindua jarida hilo  katika kikao cha mapitio ya mpango mkakati wa pili wa mahakama wa mwaka (2020/2021) hadi 2024/2025) kupitia mradi wa maboresho  ya mahakama awamu ya pili,Jaji wa mahakama ya Rufani ya Tanzania Augustine Mwanja alisema jarida hilo linaielezea historia ya mahakama ya rufani ya Tanzania tangu kuanza kwake mwaka 1979 kufuatia kuvinjika kwa shirikisho la jumuiya ya Afrika ya mashariki.



Aidha alisema hapo awali kulikuwa na mahakama ya rufani ya Afrika ya mashariki kwa nchi tatu ikiwemo Kenya, Tanzania na Uganda na baada ya kuvunjika shirikisho hilo ndipo kila nchi iliweza kuanzisha mahakama yake ya rufani.



"Jarida hili pia linaeleza utendaji wa mahakama ya rufani na hii ni kwa ajili ya kuwapa uelewa wadau wote wa mahama ya rufani inavyotenda kazi ikiwa moja wapo ni namna ya kufikia maamuzi na litaondoa maswali kwa wananchi wanaojiuliza juu ya utendaji wa mahakama ya rufani,"alisema Jaji Mwanja.



Alisema jarida hilo pia linaonyesha ufanisi wa mahakama ya rufani kwa mwaka unaohusika lengo ni kuwafanya wadau wote wanasheria na wasiokuwa wanasheria kuelewa hasa utendaji wa mahakama ya rufani.



Jaji Mwanja alisema sasa hivi ufanisi wake ni asilimia 73 ya kesi zote zinazofikishwa katika mahakama hiyo.



Kwa upande wake Msajili wa mahakama ya Rufani ya Tanzania,Kevin Mhina alisema jarida hilo  ni la mwaka 2021 ambalo limewekwa takwimu zote mwaka huo pamoja na historia ya mahakama hiyo,changamoto na mtarajio ya miaka inayofuata.



Naye Jaji kiongozi wa Mahakama kuu ya Tanzania,Mustapher Siyani alisema pamoja na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali  ya mahakama nchini ni vyema ikaaksi na huduma zinazotolewa pamoja na kuhimarisha matumizi ya Tehama katika kazi za kila siku.



Jaji Siyani alisema matumizi ya Tehama yataokoa gharama za uendeshaji wa mahakama pamoja na muda kwa wananchi na watendaji wa mahakama.



Mtendaji Mkuu wa mahakama ya Tanzania Prof.Elisante Ole Gabriel alisema mkutano huo unauwakilishi wa wajumbe 240 kutoka kada mbalimbali kuanzia kada ya utumishi wa ukarani hadi ngazi ya majaji ikiwa lengo ni kuhakikisha watu wanafahamu kinachosemwa.



"Jambo la kimkakati ambalo tumeligundua ni pamoja na ushirikishwaji wa wananchi na watendaji wa mahakama ikiwa kwenye mpango mkakati wa pili unazaidi ya sh.bilioni 417 ambapo fedha za maboresho ambazo zimepangiwa ni zaidi ya dola za kimarekani milioni 90,"alisema Mtendaji Mkuu wa Mahakama.



Prof.Gabriel alisema eneo lingine ni uhamasishaji na utoaji elimu kwa umma kupitia vyombo mbalimbali ikiwemo viongozi wa dini hivyo anaipongeza mahakama ya rufani ikiwa hayo yote ni maboresho ya mpango mkakati wa pili.

Share To:

Post A Comment: