Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) leo tarehe 7 Machi 2022 amezindua Bodi ya Wakurugenzi ya Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC) katika hafla fupi iliyofanyika jijini Arusha. 

Akizungumza katika uzinduzi huo wa Bodi ya Wakurugezi, Waziri Mulamula ameeleza Wizara na Serikali kwa ujumla inaimani kubwa kuwa kutokana na taalamu, uzoefu na uadilifu wa wajumbe wa bodi hiyo wataiongezea AICC ufanisi na tija. “Wote tunafahamu vyema katika kipindi cha miaka miwili ya hivi karibuni Dunia imepitia changamoto ya janga la UVIKO-19 ambalo limeathiri biashara nyingi  duniani ikiwemo  Sekta ya Mikutano ya Kimataifa, hivyo kutokana na weledi wa wajumbe wa bodi hii kwa kushirikiana na Wafanyakazi bila shaka mtaenda kubuni njia mbadala za kuongeza mapato” amaeeleza Waziri Mulamula.

Kwa upande wake Balozi Begum Karim Taj ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi hiyo sambamba na kuzishukuru mamlaka za uteuzi kwa kuwaamini kuingoza AICC, ameelezea utayari wa Bodi ya Wakurugenzi hiyo katika kutimiza matarajio ya Serikali ya kuhakikisha AICC inaongeza ufanisi na kuleta tija nchini. “Tupo tayari kuifanya kazi iliyoko mbele yetu ya kuhakikisha AICC inaendelea kufanya kazi kwa weledi na ubunifu, kuitangaza nchi na wakati huo huo kuhakikisha mapato yake yanaongezeka. Hii ni pamoja na kuongeza msukumo katika kudai madeni ambayo Kituo kinadai kwa wateja wake na kuhakisha yanalipwa kwa wakati ili kuendelea kutoa fursa kwa AICC kufanya kazi kwa ufanisi zaidi”. Balozi Begum Taj

Aidha, Waziri Mulamula amewahakikishia ushirikiano Wajumbe wa Bodi hiyo katika kutimiza malengo waliyojiwekea.

Wakati huohuo Waziri wa Mambo ya Nje wa ushirikiano w Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Liberata Mulamula, leo Tarehe 7 Machi 2022 amefanya mazungumzo na Mkurugenzi wa UN Women wa Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika Dkt. Maxime Houinato jijini Arusha.


Mazungumzo yao yalilenga kukuza ushirikiano uliopo baina ya Serikali ya Tanzania na UN Women. Katika Mazungumzo hayo, Dkt. Houinato ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendeleza jitihada zake za kumkomboa mwanamke katika nyanja zote za maendeleo.

Dkt. Houinato amemuhakikishia Mhe. Balozi Mulamula kuwa UN Women inathamini mchango wa Tanzania katika kuleta usawa wa kijinsia barani Afrika na itaendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha mipango yake ya kumkomboa mwanamke nchini inatekelezwa kwa ufanisi.

Kwa upande wake Mhe. Balozi Mulamula ameishukuru UN Women kwa kuendelea kuwa mdau mkubwa wa masuala ya wanawake Nchini. Aliishukuru UN Women kwa kuendelea kutekeleza majukumu yake yanayolenga kuleta usawa wa kijinsia, kuwainua wanawake kiuchumi na kupambana na ukatili wa kijinsia.

Balozi Mulamula ameihakikishia UN Women utayari wa Serikali kuendelea kushirikiana nao katika kuhakikisha kuwa Wanawake wanapiga hatua za kimaendeleo. 

Dkt. Houinato yuko Nchini kushiriki katika maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani ambayo hufanyika Tarehe 8 Machi ya Kila mwaka.
Share To:

Post A Comment: