Naibu Waziri Wa Kilimo Mh.Anthony Mavunde amekitaka kituo cha  Utafiti wa Kilimo (TARI) Seliani kuhakikisha kinakuja na mkakati na ubunifu katika uzalishaji wa mbegu bora na kuongeza maeneo zaidi ya uzalishaji mbegu ili kusaidia kukuza zao la ngano hapa nchini kwa kuongeza uzalishaji kutoka tani laki 1 zinazozalishwa hivi sasa.

Naibu Waziri Mavunde ameyasema leo Jijini Arusha wakati wa ziara yake ya kukagua shughuli za kituo cha TARI Seliani ambacho kina jukumu la msingi la utafiti wa mazao ya ngano,shayiri na maharage.


“Lazima tuhakikishe tunapunguza uingizwaji wa ngano nchini kwa sisi kama nchi kuzalisha ngano kwa wingi,na ninyi TARI Seliani ndio mna jukumu hili kubwa la utafiti na ugunduzi wa mbegu bora kwa lengo la kuongeza tija na uzalishaji wa ngano nchini.

Wataalamu na watafiti mliopo hapa kama kuna heshima kubwa mtaipata ni kusaidia uzalishaji wa ngano hapa nchini kukua na kuipunguzia nchi gharama kubwa ya fedha ya kuagiza ngano nje ya nchi.Lazima utaalamu wenu na elimu mlizonazo zikatafsiriwe katika maendeleo ya mkulima na kilimo cha nchi hii.


Hakikisheni mnatenga eneo kubwa zaidi la shamba za uzalishaji mbegu bora za ngano,mtenge bajeti ya mifumo ya umwagiliaji badala ya kutegemea mvua ilivyo hivi sasa, na maeneo hayo yatafutieni hati miliki zake na lazima yawekewe uzio ili kuyatenganisha na shughuli za kibinadamu na wanyama.


Sisi kama Wizara tutakuwa tayari kutoa ushirikiano mkubwa ili malengo haya ya kukuza sekta ya kulima kupitia zao la ngano kuona yanafanikiwa,na hasa katika eneo la bajeti ya kusimamia vituo hivi vya utafiti wa kilimo” Alisema Mavunde


Naye Kaimu Mkurugenzi  wa kituo cha TARI Seliani,*Ndg. Rose Ubwe* ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi *wa Rais Samia Suluhu Hassan* kwa kuendelea kuongeza bajeti ya fedha za utafiti hadi kufikia *11.7 bilioni* kwa mwaka 2021/22  na kuahidi kutekeleza maagizo yote yaliyotolewa kwa mustakabali wa maendeleo ya zao la ngao hapa nchini na hasa katika kuongeza uzalishaji kupitia tafiti mbalimbali na kanuni bora za kilimo.

Share To:

Adery Masta

Post A Comment: