Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini Anthony Mavunde leo ameshiriki pamoja na wananchi katika uchimbaji wa msingi wa ujenzi wa zahanati katika mtaa wa Sogeambele kata ya Nzasa,Jijini Dodoma.


Katika zoezi hilo la ujenzi wa zahanati Mfuko wa Jimbo la Dodoma Mjini umetoa Tsh 11,000,000 kuanzisha ujenzi huo wa zahanati inayojengwa na wananchi wakishirikiana na Mbunge Mavunde.


Akizungumza na wananchi,Mbunge Mavunde amewaahidi wananchi hao kukamilika kwa haraka ujenzi wa zahanati hiyo ili ianze kutoa huduma kwa wananchi wa mtaa huo ambao hutembea umbali mrefu kupata huduma za afya.


“Huduma ya Afya ni huduma muhimu sana,ni sera ya serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kusogeza huduma za afya karibu na wananchi,ndio maana na sisi kupitia Mfuko wa Jimbo tumeamua kuunga mkono jitihada hizi za wananchi za ujenzi wa zahanati.


Zahanati hii ikikamilika itasaidia kutoa huduma kwa wananchi zaidi ya 5000 katika eneo la Sogeambele na maeneo ya jirani” Alisema Mavunde


Katika hatua nyingine Mbunge Mavunde ameahidi kushirikiana na wananchi kuanza ujenzi wa Sekondari Mpya katika eneo hilo ili kuwapunguzia mwendo watoto wa shule ambao wanatembea umbali mrefu kufuata shule ya sekondari eneo la Chihanga pamoja na kuchangia matofali 1000 kwa ajili ya ujenzi wa ofisi za walimu shule ya Msingi Sogeambele.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi,Diwani wa Kata ya Chihanga Alice Kitendya amemshukuru Mbunge Mavunde kwa kuwaunga mkono katika shughuli za maendeleo katika kata hiyo na kuahidi kumpa ushirikiano katika utendaji kazi wa kuwaletea maendeleo wananchi.


Share To:

Post A Comment: