Na Joachim Nyambo.


 


“WATOTO wadogo ili kumfanya ajisikie vizuri na kuyapenda mazingira lazima  umtengenezee ukaribu kati yake na wewe… usimchukulie kama ni mtoto..mchukulie kama ni mtu unayeweza kukaa naye..ukaongea nae vitu na  akakuelewa au mkaelewana.”


 


“Hivyo ukaribu kati ya wafanyakazi na watoto ni jambo linalowafanya watoto wasijisikie ukiwa wanapokuwa kwenye mazingira haya.Lakini jambo jingine ni miundombinu ya shule..hapa wana maeneo mengi ya michezo.”


 


Ni kauli alizotoa Mkuu wa Shule ya awali na ya msingi ya Hollyland Pre & Primary school iliyopo katika Mamlaka ya Mji mdogo wa Makongolosi,wilayani Chunya mkoani Mbeya Mwalimu Yona Mwakalinga.Alibainisha haya alipozungumza na mwandishi wa makala haya juu ya changamoto ya baadhi ya watoto kuyakataa mazingira ya shule wanapopelekwa na wazazi.


 


Mara kadhaa imekuwa ikishuhudiwa baadhi ya watoto husani wanaokwenda kuanza madarasa ya awali na darasa la kwanza wakigoma kubaki shule na kutaka kuambatana na wazazi au walezi waliowasindikiza ili warudi wote majumbani.Uchunguzi unaonesha hali hii hujitokeza zaidi kwa wanafunzi wanaokwenda kubaki katika shule za bweni.


 


Makala haya ya leo yamelenga kuangazia sababu hasa zinazopelekea watoto hawa kutotaka kubaki shuleni na kutaka warudi nymbani.Umri wao mdogo waweza kuwa sehemu ya sababu ya kutotaka kubaki shule.Lakini wadau mbalimbali wanasema mazingira yanapokuwa si rafiki kwa mtoto hususani aliye katika umri mdogo humtisha na kutamani kurudi nyumbani.


 


Zipo sababu pia za mtoto kutamani kuwa karibu na wenzake aliozoeana nao iwe ni ndani ya familia yake au majirani.Upendo wa wazazi pia humfanya mtoto ahisi kubaki shule ni kuwa mbali na watu aliowazoea.


 


Lakini mwalimu Mwakalinga anasema yapo mazingira yanayoweza kumfanya mtoto akasahau hayo yote na kupenda kubaki shuleni.Sambamba na maelezo yake ya awali anasema mazingira ya shule yaliyo rafiki ni kivutio kwa watoto hasa wadogo.Hii ni pamoja na uwepo wa miundombinu ya michezo katika eneo la shule.


 


“Sisi hapa ni tofauti na huenda mazingira yanawavutia zaidi.Hapo nje ukiangalia kuna maeneo mengi ya michezo..Lakini pia tunao utaratibu watoto wanapokuwa hawako kwenye  vipindi vya darasani huwa tuna wawekea nsinema za picha za wanyama pamoja na vitu vingine vinavyomfanya mtoto asione kama yuko sehemu ambayo  si sahihi kwake.”


 


Mku huyo wa shule anasema watoto wamekuwa wakifurahishwa sana na mambo hayo.Anaongeza kuwa suala la kuwashirikishwa waatoto kwenye suala la uandaaji wa aina ya vyakula wanavyotaka kula ni kichocheo kingine cha kumfanya mtoto aone shuleni hakuna utofauti na nyumbani kwakuwa hupata wasaa wa kuchagua wanachokipenda.


 


“Tuna utaratibu wa kwa kila wiki tunatoa siku moja ya watoto kuchagua kitu wanachotaka kupikiwa wale.Wanachopendekeza uongozi unafanya utaratibu kinapatikana.Lakini pia si wakati wote watoto wanakaa hapa kila inapofika kmwisho wa wiki tunawauliza wanataka kwenda wapi kutembea wanacheza na baadaye kurudi shule.”


 


Anasema kwa kuwafanyia hayo watoto wanajikuta wanapenda zaidi kuwepo shuleni kwakuwa wanaona hata wakiwa nyumbani hakuna kitu cha thamani wanachokipata kilicho na utofauti mkubwa na shule.


 


Mwalimu huyo anasema suala la watoto wadogo kuyakubali mazingira ya shule au kuyakataa si kwa wale wanaokwenda kuyaanza maisha ya shule pekee,lipo hata kwa waliokwishaanza masomo.Wapo wanaoweza kukataa wanaporejeshwa baada ya kumalizika kwa likizo.


 


“Watoto wanaoweza kukataa shule si wageni pekee wanaokuja kuanza masomo...hata waliokwishakuwa wenyeji iwapo mazingira si rafiki.Sisi hapa kuna wakati hata wazazi wanatupigia simu kutuulizia tunawapa nini watoto..mtotoa anafika leo nyumbani anapokwenda likizo kesho yake anawaambia anataka kurudi shuleni.Ni kwa sababu ya mazingira rafiki.”


 


“Na mazingira yanawafanya watoto kulilia kuja shule.Mfano mdogo sisi hapa tumekuwa tukipokea watoto wa umri wa miaka miwili lakini juzi hapa tumepokea mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi nane hayafikisha miaka miwili ypo anasoma darasa la awali.”


 


“Lengo la mzazi alikuwa anamleta mtoto wake anayesoma darasa la pili hapa aliyetokea likizo lakini mtoto alivyofika akaona mabembea hapo akaona wenzake wanavyocheza akaanza kulilia.Ikabidi mzazi aseme basi huyu naye namuacha..hii ni kwa sababu mazingira yenyewe hayawezi kumtia shaka mzazi.” Anasema Mwalimu Mwakalinga.


 


Mkuu huyo wa shule anasema ushirikiano wa wazazi na walezi wa wanafnzi ikiwemo ushauri ambao wamekuwa wakiutoa wanapowatembelea watoto wao shuleni hapo huimarisha uhusiano baina ya wafanyakzi na watoto kwakuwa hapo pia walimu hupata wasaa wa kuelezea dalili za kitabia na kiafya wanazoziona kwa kila mtoto na kujadili kwa pamoja namna ya kuzifanyia kazi.


 


Sophia Mwanautwa ni Diwani wa viti maalumu na pia miongoni mwa wazazi ambao watoto wao wanasoma katika shule hii.Anasema mazingira rafiki hususani yenye kuwapa fursa ya watoto wadogo kujifunza kwa kupitia michezo ya aina mbalimbali yanawafanya watoto kuwa na furaha wakati wote.


 


“Ukipita utakuta watoto wanacheza na wanaonesha kuyafurahia mazingira ya shule.Mimi nafikiri kinachowavutia watoto si michezo pekee hata uwepo wa michoro ya wanyama na pia vinyago vya wanyama ni kivutio kingine.”


 


“Tunatamani mazingira kama haya tuyaone pia kwenye shule zetu za serikali.Nafikiri ni wakati kwetu sisi madiwani kufanyia kazi wazo hili ili kusiwe na utofauti wa maisha ya shule kwa watoto wa madarasa ya awali.Kama huku wanafurahia mazingira rafiki ya shule basi na kwenye shule za serikali nako watoto wasibaki wapweke.” Alisema Diwani huyo.


 


Listaa Masumaye na Edith Jairos ni wakazi katika mji wa Makongolosi ilipo shule hii.Wanasema mazingira rafiki ya shule yanayowaweka wanafunzi kwenye ujifunzaji rafiki umekuwa chachu ya wakazi wa eneo hili kuanza kuchangamkia elimu kwa kuwapeleka watoto shule tofauti na ilivyokuwa awali walipowaskumia kwenye shughuli za uchimbaji madini.


 


Aika Temu ni afisa ustawi wa jamii wa mkoa wa Mbeya na pia mmoja wa wadau kutoka mkoani hapa waliohudhuria uzinduzi wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya awali ya mtoto(PJT-MMMAM) unaotekelezwa katika kipindi cha mwaka 2021/22 hadi 2025/26 uliozinduliwa mwishoni mwa mwaka jana jijini Dodoma.


 


Programu hii inalenga imelenga  kuwekeza moja kwa moja kwenye maendeleo ya mwanadamu kwa kukuza malezi jumuishi yenye tija katika uchumi kwa kuhimiza ushiriki wa sekta mbalimbali kutoa malezi jumishi kwa kuzingatia vipengele vitano.


 


Aika anasema kwa kuwa fursa za ujifunzaji wa awali na malezi yenye mwitikio ni sehemu ya vipengele vitano vya malezi jumuishi uwekezaji wa miundombinu rafiki kwa watoto mashuleni ni jambo linalopaswa kuzingatiwa.


 


Afisa huyo pia anasema vipengele vingine pia vya mpango huo vya Lishe bora,Ulinzi na usalama pamoja na Afya bora vinapaswa kuzingatiwa hussani kwa watoto wa madarasa ya awali wanaokaa hosteli wakiwa mbali na wazazi wao.Hivyo walimu na wafanyakazi wengine kwenye taasisi husika ni muhimu wakawa na uelewa wa kutosha juu ya vipengele hivyo muhimu.


 


Anasisitiza kuwa mambo yanayopaswa kuzingatiwa katika ubora wa huduma ni kupatikana kwa malazi safi, chakula bora, usalama na utaratibu mzuri wa usafi kwa watoto. Kadhalika, ubora unaweza kumaanisha namna mazingira ya shule yanayolinda faragha na hadhi ya mtoto.


 Share To:

Post A Comment: