Kutokana na mabadiliko ya mtindo wa maisha, watu wengi hawapati muda wa kutosha wa kupumzika. Mara nyingi mtu anapozidiwa hupunguza zaidi muda wa kupumzika ili akamilishe majukumu yake.

Ni wazi kuwa watu wengi hawafahamu umuhimu wa kupumzika, ndiyo maana hawatengi muda wa kutosha wa kupumzika. Ni ukweli usiopingika kuwa kupumzika kuna manufaa makubwa sana kwenye miili na utendaji wetu wa kazi kila siku.

Ikiwa unataka kuboresha utendaji wako wa kazi pamoja na afya yako, fahamu faida 10 za kupumzika.

1. Huongeza uwezo wa kumbukumbu

Ubongo wa mwanadamu unahitaji kupumzika ili uweze kujijenga na kufanya kazi vyema. Ikiwa mtu hatapata muda wa kutosha wa kupumzika, uwezo wake wa kutunza kumbukumbu utapungua.

Pia utafiti uliofanyika umebaini kuwa kutokupumzika huongeza kiasi fulani cha protini kwenye ubongo ambacho huchangia katika kutokea kwa maradhi ya Alzheimer (Ugonjwa wa kupoteza kumbukumbu).

2. Huondoa hatari ya kupata kiharusi

Kiharusi ni ugonjwa unaosababishwa na kupasuka kwa mishipa midogo ya damu kwenye ubongo; hili husababisha damu kuvuja ndani ya ubongo.

Utafiti uliofanyika umebaini kuwa uchovu hasa ule unaoambatana na msongo wa mawazo, unaweza kusababisha kupasuka kwa mishipa inayopeleka damu kwenye ubongo na kisha kusababisha ugonjwa wa kiharusi.

3. Hulinda afya ya moyo

Kupumzika kuna manufaa makubwa kwenye afya ya moyo wako. Ni wazi kuwa kasi ya usukumaji wa damu wakati wa kufanya shughuli mbalimbali ni tofauti na wakati unapokuwa umepumzika.

Hivyo basi, unapopata muda wa kupumzika unaupa moyo wako nafasi ya kupunguziwa mzigo wa kusukuma damu kwa kasi, ambao umeubeba wakati ulipokuwa unafanya shughuli mbalimbali.

4. Hutoa muda wa mwili kujijenga

Miili yetu inahitaji kujijenga kila mara hasa baada ya shughuli nyingi. Kwa njia ya kupumzika utaweza kuupa mwili wako nafasi nzuri ya kujijenga na kurejeshha tena nguvu iliyotumika wakati wa shughuli mbalimbali.

5. Huongeza hamasa ya utendaji

Nani anapenda kufanya kazi akiwa amechoka? Naamini hakuna. Kupata muda wa kutosha wa kupumzika kutakuwezesha kujisikia vizuri na kuwa tayari kutekeleza majukumu yaliyoko mbele yako.

Ikiwa basi unataka kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa, ni muhimu kuhakikisha unapata muda wa kutosha wa kupumzika.

6. Huimarisha misuli

Tunapopumzika misuli yetu inajijenga na kurudisha ute wake uliopotea wakati wa shughuli mbalimbali. Hivyo ni muhimu kuhakikisha kila baada ya kazi tunapata muda wa kutosha wa kupumzika ili tuboreshe afya za miili yetu.

7. Huimarisha kinga mwili

Kinga mwili ni muhimu sana kwani hutuwezesha kukabiliana na magonjwa. Kwa njia ya kupata muda wa kutosha wa kupumzika tunatoa nafasi kwa mfumo mzima wa kinga mwili kujijenga na kujiimarisha.

8. Huondoa msongo wa mawazo

Chanzo kimojawapo cha msongo wa mawazo ni uchovu, na chanzo kimojawapo cha maradhi mbalimbali ni msongo wa mawazo.

Hivyo ni muhimu kuhakikisha tunapumzika ili akili na fikra zetu zijisafi na kutuepusha na tatizo la msongo wa mawazo.

9. Hutuwezesha kula vizuri

Ni ukweli usiopingika kuwa tukiwa tumechoka hatuwezi kula vizuri. Hivyo kupata muda mzuri na wakutosha wa kupumzika kutakuwezesha kula chakula vyema.

10. Huepusha ajali za barabarani

Je ulishasikia ajali zilizosababishwa na madereva wanaosinzia? Uchoovu na kukosa muda wa kupumzika (hasa kulala) humfanya mtu akose utulivu na uwezo wa kumudu chombo anachoedesha.

Hivyo ni muhimu kwa madereva na watu wote wanaotumia vyombo vya usafiri kuhakikisha wanapata muda mzuri na wakutosha wa kupumzika.

Neno la Mwisho:

Naamini hutopuuzia tena swala la kupumzika kwani umeona jinsi lilivyo na umuhimu mkubwa. Kumbuka kuwa ili uwe na ufanisi mzuri katika kazi au kile unachokifanya unahitaji kuhakikisha mwili na akili yako viko katika hali nzuri. Je wewe huwa unapumzika?  Acha kuchakaza mwili wako sasa; tenga muda wa kutosha wa kupumzika.

Share To:

Post A Comment: