Na Ahmed Mahmoud 

Wakuu wa Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamepiga kura kuridhia Jamhuri Ya Kidemokrasia Ya Kongo (DRC), kuwa mwanachama wa Saba wa Jumuiya hiyo. 


 Viongozi hao wameridhia suala hilo kupitia kura zilizopigwa wakati wa mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao, ukiongozwa na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta. 


Mwezi Disemba mwaka 2021, wakuu wa Jumuiya hiyo walipokea ripoti ya uhakiki wa utayari wa DRC kujiunga na EAC na kuwataka mawaziri wa Jumuiya hiyo kuharakisha mchakato wa majadiliano ya mkataba ili kuiwezesha DRC kuwa mwanachama na kuiwasilisha mapema mwaka wa 2022 wakati wa mkutano wa kawaida wa wakuu wa nchi wanachama wa jumuiya hiyo DRC ikiwa nchi ya saba kujiunga na Jumuiya hii, kwa sasa ndiyo nchi inyoongoza kwa idadi kubwa ya watu ndani ya nchi zilizopo EAC, ikiwa na watu takribani Milioni 92 jambo litakalopanua mzunguko wa biashara na upatikanaji wa masoko ya bidhaa zinazozalishwa ndani ya Jumuiya.


Lakini pia Tanzania itanufaika hasa katika ukuaji wa matumizi ya bandari, jambo litakalo chochea ukuaji wa uchumi nchini Tanzania pamoja na nchi zilizo ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kiusalama, DRC kudhiriwa kuwa ndani ya EAC itasaidia sana mapambano dhidi ya makundi ya waasi ambao wamekuwa wakitajwa kujificha ndani ya misiti mikubwa DRC na kuzishambulia nchi kama Rwanda na Uganda. Kwa Upande wake Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dkt.Peter Mathuki akizungumza na waandishi wa habari alisema Leo ni siku kubwa ya heshima kwa eac kuialika rasmi Congo kuwa mwanachama mpya wa EAC.

"Siku ya Leo kwetu ni siku kubwa ya heshima kuialika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki na wakuu wa nchi za Eac wameitisha rasmi Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kuwa mwanachama wa Jumuiya hiyo" Amesema ni Furaha yao na wananchi kupitia kujiunga kwa Congo DRC kutaongeza fursa za kiuchumi na kibiashara katika kusafirisha bidhaa kuanzia bahari ya Hindi hadi bahari ya Atlantiki. 

 Ameeleza kwamba nchi hizo zikikubaliana kuondoa vikwazo mipakani katika biashara zitaongeza nafasi kwa wananchi wa Jumuiya hiyo. Kwa Sasa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinakadiriwa kuwa wa raia wapatao 193 milioni hivyo kujiunga kwa DRC Congo kutaongeza idadi hiyo nakufikia watu milion 280 na hivyo kufanya muingiliano wa kibiashara kuwa mkubwa zaidi. Akizungumzia masuala yakiusalama katika nchi hiyo amesema kwamba nchi hizo zitafanya jitihada za pamoja kuunganisha nguvu kuhakikisha wanadumisha usalama na amani katika nchi hiyo.

"Sisi kwa pamoja tutajitahidi kuwasaidia kuona Jamhuri ya Congo inaondokana nachangamoto za kiusalama zilizopo katika nchi hiyo kwa umoja wetu kama nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki" Waheshimiwa maraisi ninapenda kutumia fursa hii kuwashukuru sana kwa kunikaribisha katika mkutano huu maalumu ambapo kwa mara ya kwanza ninazungumza kwa niaba ya wananchi wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo kama mwanachama mpya wa jumuiya ya Afrika Mashariki.

” Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi akizungumza katika kikao cha wakuu wa nchi wa jumuiya ya Afrika Mashariki akiwakilisha nchi yake kama mwanachama mpya wa jumuiya hiyo.


 Pamoja na mambo mengine Tshisekedi amesema anatarajia kwamba kuwa ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki kutaisaidia nchi yake kuwa na ulinzi na usalama hasa eneo la Mashariki mwa Congo ambalo linakumbwa na machafuko. 


Kwa Upande wake Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kwamba Taifa la Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo lililo kusini mwa jangwa la Sahara lina watu wanaofikia milioni 90 na ni taifa la pili kwa ukubwa barani Afrika baada ya Algeria iliyoko kaskazini mwa Afrika. 


Katika kikao cha cha leo wakuu wa nchi kwa pamoja wameikaribisha Congo na kuonesha matarajio ya kila upande kufaidika, “Tanzania inasema karibu sana DRC. Ni matumaini yangu kwamba DRC inauharakisha mchakato wa kukamilisha makubaliano yaliyo katika mkataba wa kujiunga, ili kuwapa wananchi wake fursa ya kufurahia matunda ya jumuiya. 

Maamuzi yenu ya kujiunga na jumuiya yatasaidia kupatikana na amani na ulinzi, umoja na mshikamano sio tu Congo bali kwa jumuiya nzima kw aujumla.” 

 Kwa sasa Jumuiya ya Afrika Mashariki imepanuka kutoka nchi sita na kuwa saba, na hiyo inatengeneza wigo mpana zaidi wa kibiashara kuanzia bahari ya hindi mpaka ya atlantiki, lakini wito wa katibu mkuu wa jumuiya ya Afrika Mashariki Dr. Peter Mathuki ni kuondolewa kwa vikwazo vyote vya kibiashara baina ya nchi wanachama. Jumuiya ya Afrika Mashariki ndio jumuiya kongwe zaidi barani Afrika, ikiundwa hivi sasa na saba ambazo ni Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo ambayo imekuwa mwanachama rasmi kuanzia leo.
Share To:

Arusha Newsroom

Post A Comment: