Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesema wizara yake itaanza ukaguzi na kuyatambua maeneo yote yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji nchini.

Dkt Mabula alisema hayo leo tarehe 9 Februari jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari ikiwa ni muda mfupi baada ya kutoka kuapishwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

‘’Maeneo haya lazima tuyafanyie ukaguzi pamoja na kuyatambua hasa yale ya vijijini ambayo ardhi yake inahitaji uhaulishaji ili kupunguza muda wa mwekezaji kusubiri pale anapohitahitaji ardhi ya kufanya uwekezaji’’ alisema Dkt Mabula

  ‘‘Vipaumbele vya Wizara haviwezi kwenda tofauti na vipaumbele vya Rais ambapo Mhe. Rais ameelekeza suala zima la uwekezaji ambapo sisi kama Wizara tutafanya ukaguzi wa maeneo yote yaliyotengwa tuyatambue na tujue wenzetu wa TIC, TAMISEMI, EPZA ardhi walionayo ni kiasi gani na wamepanga kufanya nini’’ alisema Dkt Mabula

Kwa mujibu wa Waziri wa Ardhi, Halmashauri kwa maana ya TAMISEMI kupitia mipango kabambe katika maeneo yao kuna maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji na wizara itataka kujua kiasi gani cha maeneo yaliyopo yamepangwa kwa kwa makusudio gani.

Dkt Mabula ambaye amechukua kijiti cha uwaziri kutoka kwa William Lukuvi alisema, jukumu la Wizara ya ardhi litakuwa ni kutwaa maeneo hayo ili yawe chini yha serikali ili muwekezaji atakapofika serikali itajua sehemu sahihi kumpeleka kwa kuwa kutakuwa na kanzidata ya maeneo husika.

‘‘Kwenye maeneo ya Vijiji kuna maeneo mengi ambayo yana fursa nzuri za uwekezaji ambapo ardhi ya vijiji inasimamiwa na Sheria Na. 5 ili iweze kumilikiwa inabidi zoezi la uhaulishaji katika maeneo yaliyokusudiwa  kuwa ya uwekezaji lifanyike kwa ukamilifu na kuwe na umiliki wa eneo ili mwekezaji atakapokuja tusianze kufanya mikutano ya wananchi ili wakubali’’ alisema Dkt Mabula .

Akigeukia suala la migogoro ya Ardhi, Dkt Mabula alieleza kuwa migogoro ya ardhi inagusa Wizara tano za Kisekta na inatokea kwa sababu hapajaweza kuwekewa mpango wa matumizi ya ardhi kwa nchi nzima na kubainisha kuwa, wizara itazungumza na Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa maana ya  halmashauri zote ili kuweza kuona kwa jinsi gani patakuwa na zoezi la maksudi kabisa la kuhakikisha kwamba walau vijiji na maeneo mengi yanapangiwa matumizi ya ardhi.

‘‘Bila kuwa na mpango wa matumizi ya ardhi migogoro haiwezi kuisha na tukipanga na kuheshishimu makubaliano yaliyowekwa katika maeneo hayo ni wazi migogoro itapungua, ili kufanikisha hili inahitaji ushirikiano wa Wizara Tano za Kisekta’’ alisema Dkt Mabula.

Kwa upande wa zoezi la anuani za makazi, Waziri wa Ardhi alisema kipaumbele cha Wizara yake itakuwa kwenda kwa kasi kubwa katika suala zima la upimaji maeneo pamoja na kutambua wamiliki wa maeneo hayo. ‘’Kwetu sisi Wizara katika zoezi la anwani za makazi limepewa kipaumbele kikubwa kwamba tukizembea tutakuwa tumekwamisha zoezi zima’’ alisema Dkt Mabula.
Share To:

Post A Comment: