OR-TAMISEMI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa amesema tangu Serikali ilipoanzisga mpango wa Elimusimsingi bila Ada jumla ya Shilingi Trilioni 1.43 zimetumika kugharamia mpango huu.


Akizungumza katika hafla ya utoaji Tuzo za Ubora wa Taaluma kwa wanafunzi, walimu, shule, Halmashauri na Mikoa yote iliyofanya vizuri kwenye mtihani ya mwaka 2021 iliyofanyika Jijini Dodoma leo hii Waziri Bashungwa amesema mpango umeongeza uandikishaji mara dufu.


“Mtakumbuka kuwa, katika miaka iliyopita, nchi yetu ilikuwa na changamoto ya fursa ya upatikanaji wa elimu, kutokana na ada na michango mbalimbali na Serikali iliamua kuanzisha Mpango wa utoaji wa Elimumsingi Bila Malipo, ambao ulianza kutekelezwa na Serikali kuanzia Desemba, 2015, kwa kuzingatia Sera ya Elimu ya Mwaka 2014, Ibara ya 3.1.5 na Ibara ya 52(a) ya Ilani ya Uchaguzi, ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015. 


Mpaka sasa, Serikali imepeleka jumla ya shilingi trilioni 1.43, kwa ajili ya kugharamia Mpango wa Elimumsingi bila Malipo” alisema Mhe. Bashungwa


Mpango wa Elimumsingi bila malipo umeleta fursa ya upatikanaji wa Elimu kwa kuongeza uandikishaji wa wanafunzi, kutokana na kuondolewa kwa vikwazo na katika mwaka 2016, jumla ya wanafunzi 2,670,125 waliandikishwa, kati ya hao wanafunzi 917,137 wa elimu ya awali, 1,386,592 wa darasa la kwanza na wanafunzi 366,396 wa kidato cha kwanza.  Aliongeza Mhe. Bashungwa.


Katika hafka hiyo Waziri Bashungwa amekabidhi Tuzo 481  kwa walengwa 437  ambao ni wanafunzi, walimu, shule, halmashauri na Mikoa iliyofanya vizuri kwenye Mtihani ya mwaka 2021.

Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: