Mkuu wa Mkoa wa Singida ambaye ni mgeni mwalikwa kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria mkoa wa Singida mwaka 2022, Dk. Binilith Mahenge akizungumza.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Singida Alu Nzowa akizungumza kwenye maadhimisho hayo

Mwakilishi wa Mawakili wote wa Mkoa wa Singida Wakili Peter Ndimbo

akizungumza.

 Mkuu wa Ofisi ya Mashtaka Mkoa wa Singida, Salige akizungumza

  Kamati ya Ulinzi na Usalama mkoa wa Singida wakishiriki kikamilifu maadhimisho hayo.

Baadhi ya viongozi mbalimbali wa dini wakiwa kwenye maadhimisho hayo.

Mahakimu na Mawakili wa Mahakama za Singida.

 Mahakimu na Mawakili wa Mahakama za Singida.

Baadhi ya Watendaji wa Mahakama mkoani hapa.

Watendaji wa Mahakama Mkoa wa SingidKundi la baadhi ya watumishi wa mahakama.

Baadhi ya wawakilishi wa Taasisi mbalimbali za serikali wakishiriki kikamilifu maadhimisho hayo.

Picha ya pamoja.

Baadhi ya wanafunzi

Vikundi vya ngoma na Burudani. 


 Kundi la picha ya baadhi ya wananchi waliohudhuria sherehe hizo.



Na Godwin Myovela, Singida

TANGU mwaka 1996, Mahakama ya Tanzania imekuwa ikiadhimisha siku ya sheria nchini kwa lengo la kuashiria kuanza rasmi kwa shughuli za mahakama kwa mwaka husika. Maadhimisho haya kila mwaka hufanyika kwa kuongozwa na tafakuri mahsusi inayojadiliwa kama dira ya utendaji kazi wa mahakama.

Nichukue nafasi hii kupongeza hatua hiyo ambayo dhahiri inalenga kuwakutanisha wadau wa mahakama na wananchi katika dhana pana ya kupeana elimu sambamba na kukumbushana mambo kadha wa kadha ili kwa pamoja na umoja kuweza kutekeleza majukumu ya utoaji haki kwa mujibu wa  viapo.

Pia kwa kutambua umuhimu wa kuifanya mahakama kufikiwa na wananchi ambao ndio walengwa wa huduma za mahakama; tangu mwaka 2017, maadhimisho haya yamekuwa yakiongezwa msisitizo kuhakikisha chombo hiki kinazingatia pamoja na mambo mengine, mambo ya ushirikishwaji wa wadau, utawala bora, uwajibikaji na matumizi bora ya rasilimali, upatikanaji wa haki kwa wakati ili kujenga imani ya wananchi.

Binafsi nitajikita kwenye eneo moja la Mahakama Mtandao katika dhima ya kauli mbiu ya mwaka huu isemayo; “Zama za Mapinduzi ya Nne ya Viwanda: Safari ya Maboresho kuelekea Mahakama Mtandao”

 

Kupitia maadhimisho ya mwaka huu tumeelezwa kwamba Mahakama Mtandao (e-judiciary) ni Mahakama inayoendesha shughuli zake zote za utoaji haki na zile za kiutawala kwa njia ya kielektroniki au kwa lugha nyepesi kwa kutumia TEHAMA (emails, simu za mkononi, internet na mitandao mbalimbali ya kijamii) kikamilifu katika shughuli zake zote.

Kwa mujibu wa mahakama huduma hiyo mpaka sasa inaendelea kufanyika kuanzia eneo la ufunguaji wa mashauri, usikilizwaji, uhifadhi wa nyaraka, utunzaji wa taarifa za kiutumishi, udhibiti wa rasilimali na mifumo ya malalamiko

Pia kuna maeneo mengi ambayo Mahakama imeyaboresha au kuyaanzisha yanayoonesha dhahiri kuwa chombo hiki kinasafiri kuelekea Mahakama Mtandao, ikiwemo uboreshaji wa miundombinu, uanzishaji wa vituo jumuishi vya utoaji haki, uanzishaji wa mahakama inayotembea na matumizi na maboresho ya Tehama.

 Hata hivyo, tumeelezwa kwamba, kwa sasa kuna faida nyingi ambazo watumiaji wa huduma za kimahakama wameanza kuzipata kutokana na uwepo wa mahakama mtandao ikiwemo; urahisi na uharaka usikilizwaji wa mashauri kuanzia kwenye uwasilishwaji wa mashauri mahakamani, usajili wa mashauri lakini pia upatikanaji wa nyaraka na taarifa za mashauri.

Wadaawa wanaweza kuwasilisha shauri bila kufika mahakamani shauri likapokelewa, likafunguliwa na mhusika akapewa mrejesho huko huko alipo. Pia shauri linaweza kuendeshwa kwa kutumia mfumo wa video. Lakini pia mahakama mtandao inapunguza gharama za uendeshaji wa mashauri kwa wadaawa, wadau na mahakama yenyewe.

Imethibitika kwa kutumia mahakama mtandao gharama za uendeshaji wa mashauri zimeendelea kupungua kwa kiasi kikubwa kwa pande zote katika shauri, na hususani kwenye nyanja ya mahakama inayotembea mpaka sasa takribani mashauri 1,208 yamesikilizwa na watu wapatao 13,668 na huduma hii.

Aidha, mahakama mtandao inaongeza uwazi katika shughuli za kimahakama. Wadaawa wanaweza kufuatilia mwenendo wa shauri kupitia mtandao bila kukutana na urasimu wa aina yoyote.

Pia mahakama mtandao inasaidia taasisi kupata takwimu sahihi za mashauri na kwa wakati. Inaongeza ufanisi katika kutekeleza jukumu la msingi la utoaji haki, na kurahisisha upatikanaji wa haki kwa wakati.

Zaidi, ni chombo cha kukusanyia mapato ya serikali ambayo hapo awali kulikuwa na upotevu mkubwa. Lakini pia taasisi inaitumia mahakama mtandao kama chombo cha kufanyia tathmini ya mtu mmoja mmoja au mahakama husika na mahakama kama taasisi kwa ujumla.

Changamoto za Mahakama Mtandao

Suala la elimu kuhusu matumizi ya huduma hiyo bado ni changamoto ikizingatiwa wananchi wengi wanashindwa kuendana na maboresho ya huduma hiyo ya kitehama kutokana na sababu za kimazingira kwa wengi hasa vijijni kukosa mawasiliano ya kimtandao huku wengine wakikosa elimu ya namna ya kutumia huduma hiyo.

Ni dhahiri, mpaka sasa kuna ombwe kubwa la wengi kupata usumbufu mkubwa hasa kwenye eneo la kusajili kesi au kufuatilia tarehe za kesi zao kutokana na kukosa simu za viganjani na vifaa vingine vinavyoendana na huduma hiyo, huku hata wengine wenye vifaa hivyo nao wakijikuta wanakosa wataalamu stahiki wa kuwaelekeza nini cha kufanya kutokana na uchache wa wataalamu wa sekta hiyo ndani ya mahakama.

Mathalani sio mahakama zote zenye TVs na vifaa vya kutosha kuweza kuendesha kesi kwa video conference hali inayopelekea changamoto ya hata namna ya kuthibitisha vielelezo vinavyotolewa kupitia huduma hiyo.

Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na chama cha mawakili nchini (TLS) kwenye eneo hilo kupitia kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria mwaka huu-mkoani hapa-imebainika, pamoja na mambo mengine, pia hata usajili wa kesi kwa njia ya mtandao bado kuna urasimu; imeelezwa hata ukisajili kwa njia hiyo bado tena utatakiwa kupeleka tena nyaraka halisi mahakamani hali inayoleta mkanganyiko kwa wananchi.

Pia upatikanaji wa mtandao kwa maeneo mengi ni changamoto huku pia wadau wengine kama mabaraza ya ardhi na tume za ajira za usuluhishi na maamuzi hawajaungwa hivyo kufifisha huduma hiyo muhimu, na chombo hicho kujikuta kikitengeneza double standard kwenye utoaji haki nchini.

Binafsi naamini na naunga mkono ushauri uliotolewa na TLS kuwa mfumo huu wa mahakama mtandao kwanza; uingizwe kwenye mtaala wa mafunzo ya wanasheria vyuoni ili iwe sehemu ya ujuzi wanaopata kabla ya kuingia kazini.

Pia, kuwe na elimu endelevu kwa mawakili waliopo kazini na wadau wengine wote wa mahakama na wananchi ili elimu hiyo anuai ieleweke ipasavyo na kwa kiwango cha kutosha kwa kila mtu kuweza kunufaika nayo.

Katika kufanikisha hilo, mahakama haina budi kuajiri wataalamu wa kutosha wa taaluma ya Habari na Mawasiliano walau kila ilipo mahakama ya wilaya ili kuwezesha watumiaji wa huduma hiyo kuwa na ufanisi katika matumizi yake.

Lakini kupitia maadhimisho hayo ilishauriwa mahakama ifanye kazi kwa ukaribu na makampuni wamiliki wa mitandao kama TTCL, Vodacom, Tigo, Halotel, Zantel kwa pamoja kufanikisha maboresho ya matumizi ya huduma hiyo ya mahakama mtandao hasa kwa maeneo ya vijijini.

Na kama maoni hayo muhimu ya wadau yatazingatiwa; basi; dhima hiyo huenda sasa ikawa ndio mwongozo sahihi kwa Mahakama ya Tanzania katika muktadha chanya wa Mahakama Mtandao yenye tija kwa wananchi kuona, kupata taarifa, maelekezo na huduma zote muhimu bila hata kufika moja kwa moja kwenye majengo ya mahakama.


Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: