******************************

Na. John Mapepele

Serikali tayari imetenga shule 56 za michezo nchi nzima ili kuibua na kukuza vipaji vya michezo kwa watoto nchi nzima.

Kauli hii imetolewa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa Februari 4, 2022 katika ubalozi wa China jijini Dar es Salaam kwenye siku ya mwaka mpya wa Taifa hilo na siku ya uzinduzi wa mashindano ya mwaka 2022 ya Olympiki ya Beijing ya majira ya baridi.

Utengaji wa shule hizo pia ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa wakati akifungua Mashindano ya Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi (UMITASHUMTA) na Sekondari (UMISSETA) kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara Juni 8, 2021 ambapo alielekeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na mambo mengine isimamie utengaji wa shule maalum za Michezo nchi nzima.

Aidha, Mhe. Mchengerwa amefafanua kwamba kutenga kwa shule hizo za michezo nchi nzima ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi Chama cha Mapinduzi (CCM) unaoitaka Serikali kuibua vipaji vya watoto ili kupata wanamichezo bora na kuimarisha michezo kwa ujumla.

Aidha, amesema hadi sasa Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya TAMISEMI na Wizara yenye dhamana ya Elimu zimesha ainisha shule hizo kwa ajili ya maboresho mbalimbali ya miundombinu ya michezo.

Ameongeza kuwa Wizara yake itahakikisha inasimamia zoezi hili kikamilifu ili kuleta Mapinduzi makubwa kwenye michezo.

Amemwomba Balozi wa China nchini Chen kuiomba Serikali yake kusaidia uboreshaji wa miundombinu ya michezo ya shule hizo ili Ilani ya CCM ambayo inaendana na ile ya Chama cha CPC cha nchini China iweze kutekelezwa.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: