Kesi ya mauaji ya mfanyabiashara wa madini, Mussa Hamis inayowakabili maofisa saba wa polisi mkoani Mtwara, imeahirishwa kutokana na kile kilichoelezwa kuwa upelelezi bado unaendelea.

Washitakiwa hao wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mtwara leo Jumanne ya Februari 22, 2022 mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Lugano Kasebele na kisha  kuahirishwa hadi Machi 8, 2022.

Waliopandishwa kizimbani ni Ofisa Upelelezi Wilaya ya Mtwara, Gilbert Kalanje, Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara, Charles Onyango, Ofisa wa Intelijensia ya Jinai Mkoa wa Mtwara, Charles Kisinza na Mkaguzi wa Polisi, John Msuya.

Wengine ni Mganga Mkuu wa Zahanati ya Polisi, Marco Mbuta, Mkaguzi wa Polisi, Shirazi Mkupa na Koplo Salum Juma Mbalu.

Awali, washitakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Januari 25, 2022 na kusomewa shitaka la mauaji ya kukusudia.

Mapema leo Jumanne, washitakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo saa 2.57 asubuhi na kufikia saa 3.26 asubuhi kesi hiyo ilikuwa imeshasikilizwa na kuahirishwa.

Kama kawaida washitakiwa hao wamefikishwa mahakamani hapo wakiwa chini ya ulinzi mkali huku ndugu na jamaa wakifurika kusikiliza shauri hilo.

Wakili wa Serikali Ajuaye Bilishanga Zegeli ameieleza mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika hivyo, kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa tena.

Hakimu Kasebele amesema kwa kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuahirisha kesi hiyo hadi Machi 8, 2022 itakapotajwa tena.
Share To:

Post A Comment: