OR-TAMISEMI


OFISI ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imeomba kibali kwa Rais Samia Suluhu Hassan cha kuajiri Walimu 7,000 ili kupunguza upungufu wa walimu wa Shule za Msingi na Sekondari nchini.


Waziri wa TAMISEMI Innocent Bashungwa aliyasema hayo  kwenye mdahalo maalum wa kujadili mafaniko katika Sekta ya elimu kwa mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan uliofanyika kwa njia ya mtandao wa Zoom jijini hapa.


Alisema ndani ya utawala wa Rais Samia tayari alishatoa kibali cha kuajiri Walimu 6,949 ambapo Walimu 3,000 walikuwa Walimu wa sayansi kwa shule za Sekondari na wameshaajiriwa na wako kwenye vituo vya kazi.


Hata hivyo, alisema katika kuendelea kutatua tatizo la uhaba wa walimu, tayari Ofisi hiyo imeomba kibali hicho kwa Rais ili aridhie kuajiriwa walimu hao.


Waziri Bashungwa alisema kwa mwaka mmoja wa Rais Samia madarakaninametoa fedha za kujenga miundombinu mbalimbali ya elimu.


“Nitumie nafasi hii kumpongeza Rais Samia kwa kuamua kuzielekeza fedha za mkopo wa IMF katika miradi endelevu na inayoonekana kama ujenzi wa madarasa 12,000 ambayo yamepunguza msongamano madarasa na wanafunzi kutembea mwendo mrefu,”alisema.


Kadhalika, alisema serikali imetoa Sh.Bilioni 30 kwenye Mikoa 10 nchini kwa ajili ya kujenga shule maalum za sayansi za wanafunzi wa kike.

 

Alisema kila Mkoa umepokea Sh.Bilioni tatu kwa ajili ya kujenga shule hizo kwenye Mkoa wa Dar es salaam, Kagera, Lindi, Pwani, Ruvuma, Shinyanga, Singida, Songwe, Tanga na Mwanza.

 

Hata hivyo, alisema kupitia mradi wa SEQUIP (Mradi wa kuboresha elimu ya Sekondari) Serikali imepeleka Sh.Bilioni 110 kwenye Kata 235 ambazo hazina Shule za Sekondari na ujenzi umeshaanza na wengine wapo hatua ya ukamilishaji wa shule hizo.


Vile vile, Waziri Bashungwa alibainisha kuwa kupitia bajeti inayoandaliwa kwa mwaka 2022/23 wataweka kipaumbele cha kukabili upungufu wa matundu ya vyoo hasa kwa shule za msingi itakayokwenda sambamba na kupunguza uhaba wa nyumba za walimu

Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: