Na. Elinipa Lupembe.


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira Mhe. Dr. Seleman Jafo amewataka wananchi wa mkoa wa Arusha, kuelekeza nguvu katika kutunza mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi, yanayosababisha ukame na ongezeko la joto duniani hususani katika maeneo mengi ya Tanzania kwa sasa.


Waziri Jafo ametoa rai hiyo, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua vyanzo vya maji vya Usa -River na Midawe katika wilaya ya Arumeru na kusema kuwa, kwa sasa matokeo hasi ya mabadiliko ya tabia nchi, yamejitokeza dhahiri huku yakileta madhara kwa jamii na mali zao.


"Ukiangalia hali ya hewa nchini imebadilika sana, joto limeongezeka kwa kasi, mfano hali ya hewa ya Arusha ilikuwa ni baridi sana, ila sasa kuna joto, joto ambalo limesababisha ukame katika maeneo mengi, ukame ambao umeanza kuleta madhara kwa watu na mali zao, ikiwemo vifo vya mifugo, jambo ambalo tunapaswa kuchukua hatua za haraka kwa kuweka mikakati thabiti ya kutunza mazingira yetu" Amesisitiza Mheshimiwa Waziri Jafo.


Licha ya Waziri Jafo, kuridhishwa na hali ya utunzaji wa mazingira hasa kwenye vyanzo vya maji, wilayani Arumeru, amesisitiza kuendelea kutunza vyanzo hivyo vya maji pamoja na kuwa na mikakati endelevu kwa kupanda miti, ikiwa ni pamoja na halmashauri kuwezesha kila mwanafunzi kuotesha mti mmoja katika shule na maeneo yanayozunguka shule zao.


Hata hivyo Waziri Jafo amezitaka halmashauri kuhakikisha zinaweka bajeti ya utunzaji na uendelezaji wa mazingira asilia, hasa kwa kuwekeza kwenye uanzishwaji wa vitalu vya miti, kuhamasisha jamii kuotesha miti kwa wingi katika maeneo yao, jambo litakalorudisha ikolojia ya mazingira, inayoanza kuharibika kwa sasa.


Aidha katika ziara hiyo, mheshimiwa Jafo amefanikiwa kuotesha miti kwa kushirikiana na wanafunzi wa shule ya sekondari Bangata halmashauri ya Arusha, katika eneo la tanki la maji Midawe linalomilikiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Arusha 'AUWSA' na kugawa miti kwa wanafunzi wa shule hiyo, kwa ajili ya kuiotesha kuzunguka eneo hilo la chanzo cha maji, chanzo kinacholisha maji kwa wananchi wa eneo la Arumeru na Jiji la Arusha.


Afisa Mazingira Bonde la Mto Pangani, Felista Joseph, amethibitihsa kupungua kwa kiasi cha maji kutokana na ongezeko kubwa la idadi ya watu na baadhi ya watu kuvamia maeneo ya vyanzo vya maji, lakini Bonde la mto Pangani linasimamia vyanzo vya maji nchini huku likiwa na jukumu la kugawa matumizi ya maji kukingana na kiasi cha maji ili yaweze kutosheleza kwa watumiaji wote bila kuleta migogoro katika jamii.


"Kiasi cha maji kilichopo kinagawanywa kwa makundi kulingana na matumizi, wapo watumiaji wa kubwa ambao ni Mamlaka za Maji Safi na Usafi wa Mazingira nchini na makampuni yanayomiliki mashamba makubwa, watumiaji wadogo wa mifereji na kubakiza kiasi cha maji kwa ajili ya mazingira na viumbe vyake" amefafanua Afisa Mazingira wa Bonde la Mto Pangani.


Naye Mkuu wa wilaya ya Aruemeru, Mhandisi Richard Ruyango, licha ya kumshukuru Mheshimiwa Waziri huyo, kwa kutembelea na kukagua hali ya utunzaji wa mazingira katika wilaya ya Arumeru, ameahidi kutekeleza maagizo na ushauri uliotolewa na Waziri huyo, kwa kuhakikisha kila mwanafunzi anapanda mti mmoja pamoja na kuongeza bajeti ya mazingira katika halmashauri zote za Arusha na Meru, huku wakiweka kipaumbele katika kuhamasisha jamii kwenye utunzaji wa mazingira hasa wananchi wanaoishi maeneo yanayozunguka vyanzo vya maji.


Katika ziara hiyo ya siku moja, Waziri Jafo ametembelea chanzo cha maji USA River, bustani ya Miti halmashauri ya Meru na chanzo cha maji na Kituo cha maji cha AUWSA kilichopo Midawe, halmashauri ya Arusha.



Share To:

Post A Comment: