Mkuu wa Mkoa Singida Dk.Binilith Mahenge akionesha darasa la Shule Shikizi ya Kudema ambayo ilijengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi. Hivi sasa shule hiyo haitatumika tena na badala yake watoto hayo watahamia katika shule yenye majengo ya kisasa yanayojengwa katika eneo hilo baada ya Rais Samia Suluhu kutoa fedha za ujenzi wa shule hizo shikizi katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi. Katikati mwenye miwani ni Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi, Yahaya Masere.
Mkuu wa Mkoa Singida Dk.Binilith Mahenge akiangalia darasa la Shule Shikizi ya Kudema lilivyokuwa kwa ndani.
Mkuu wa Mkoa Singida Dk.Binilith Mahenge (kulia) akizungumza na viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Itigi wakati wa ziara yake ya siku moja ya kukagua ujenzi wa shule shikizi aliyoifanya juzi. Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, John Mgalula, Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Rungwa, Stewart Kibona na Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi, Yahaya Masere. 
Muonekano wa darasa la Shule ya Sekondari ya Rungwa katika hatua za mwisho za ujenzi wake.
Muonekano wa Moja la darasa lililojengwa kwa miti na kuezekwa kwa nyasi la Shule Shikizi ya Kudema..


Na Dotto Mwaibale, Itigi, Singida


MKUU wa Mkoa Singida Dk.Binilith Mahenge ameridhishwa na ukamilishaji wa ujenzi wa vituo shikizi kwa ajili ya kusomea watoto katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi ambapo ameutaka uongozi wa halmashauri hiyo kukamilisha haraka umaliziaji wa vituo hivyo ili kutoa fursa kwa watoto kuanza kuvitumia kuanzia kesho.

Mahenge aliyasema hayo juzi wakati alipofanya ziara ya siku moja Kata ya Rungwa wilayani humo ya kukagua vituo hivyo na shule za sekondari shikizi ambazo ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 90.

"Kazi iliyobakia ni kumalizia vitu vidogo vidogo vilivyo bakia nawaombeni muvimalizie haraka iwezekanavyo ili Jumatatu Januari 17 vianze kutumiwa na watoto wetu ambao tayari wamekwisha andikishwa" alisema Mahenge.

Mahenge aliwataka Watendaji wa vijiji na vitongoji na madiwani kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha kazi zilizobakia kama kufanya usafi maeneo yanao zunguka shule hizo wanazifanya kwa pamoja.

Dkt.Mahenge alisema Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya ujenzi wa shule, barabara na vituo vya afya  hivyo kila mwananchi anawajibika  kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali wakati wa kutekeleza miradi hiyo ambayo pia imetoa fursa ya ajira.

Katika ziara hiyo Dk. Mahenge alichangia Sh. 4 Milioni kwa ajili ya ujenzi wa matundu manne ya vyoo katika vituo shikizi vya Kudema na Itaga ambapo Mbunge wa Jimbo la Manyoni Magharibi Yahaya Masare alichangia Sh.1 milioni.

Mahenge ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu kwa kutoa fedha kwa halmashauri hiyo ambazo zimesaidia kuongeza miundombinu ya elimu ambapo zitawaondolea adha wanafunzi waliokuwa wakitembea umbali mrefu kwenda kwenye maeneo yaliyokuwa na shule.  

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Itigi John Mgalula alisema vituo hivyo shikizi ni muhimu kwa kuwa kituo kimoja kina watoto zaidi ya 350 hivyo vitawasadia watoto wenye umri mdogo ambao wanaokaa mbali na shule.

Mgalula alimuomba Dk. Mahenge baadhi ya vituo hivyo shikizi kubadilishwa na kuwa shule kamili ambpo alitumia nafasi hiyo kuishukuru Serikali kwa kutoa fedha hiyo kwa halmshauri hiyo.

Vituo shikizi vilivyotembelewa na kukaguliwa ujenzi wake ni Shule shikizi ya Kijiji cha Nkana ambacho kinajenga madarasa matatu, shule shikizi ya Kudema ambayo inajenga madarasa madarasa 8, shule shikizi ya Itaga ambayo inajenga madarasa 8 na Shule ya Sekondari shikizi ya Ngirimalole iliyopo Kata ya Mwamagembe.

Shule zingine ambao ujenzi wake unaendelea ni Sekondari ya Rungwa ambapo vinajengwa vyumba vitatu, vyumba vitatu ambavyo vinajengwa Shule ya Sekondari Kalekwa, Vyumba vitatu Shule ya Sekondari ya Mitundu na vyumba vitatu vya madarasa Shule ya Sekondari ya Mgandu.

Share To:

dotto mwaibale

Post A Comment: