Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde  ametembelea kiwanda cha kuchakata viazi mringo  na kuwahimiza wakulima  mkoani Iringa kuchangamkia fursa hiyo ya kilimo cha mkataba pindi kiwanda hicho kitakapoanza kazi.

 Mavunde ameyasema hayo leo tarehe 25 Januari, 2022 alipotembelea kiwanda cha kutengeneza chipsi na crips kinachomilikiwa na Kampuni ya SAI Energy and Logistics Services Ltd kilichopo Manispaa ya Iringa na kupata maelezo kutoka kwa mwekezaji wa kiwanda hicho, Ndg. Rajan Mwaruhaa ambaye alieleza kuwa kiwanda hicho kina zaidi ya miaka 3 kimesimama uzalishaji kutokana na ukosefu wa malighafi, ambayo inahitajika kuzalishwa na wakulima kwa kuotesha mbegu bora ya viazi mviringo iliyosafishwa na hivyo kuwa na tija kubwa na kwamba kiwanda hicho kitahitaji tani 18,000 za viazi mviringo kutoa fursa kwa wakulima 5000 watakaokuwa kwenye mfumo wa block farming.


Akiwa kiwandani hapo, Mavunde alisisitiza kuwa uwepo wa kiwanda hicho ni fursa ya ajira kwa wananchi hususan makundi maalum ya wanawake na vijana, hivyo ni muda muafaka kuitumia ipasavyo.


"Nitakuomba Mohammed Moyo, Mkuu wetu wa Wilaya ya Iringa, utusaidie kukaa na wataalam hapa ili mtenge eneo ambalo tutaanzisha shamba la mfano la kilimo cha viazi mviringo kwa kutumia vizimba (block farming) ili wakulima wetu waweze kunufaika na soko linaloletwa na kiwanda hiki" aliongeza Mhe. Mavunde.


Wakati huo huo, Mavunde ametoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) ili kesho asubuhi tarehe 26 Januari, 2022 wataalam wa viazi mviringo wafike kwa mwekezaji huyo ndugu Rajan na kuhakikisha wanatatua haraka changamoto hiyo ya mbegu.


Wakizungumza kwa nyakati tofauti Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mohammed Moyo na Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini Jesca Msambatavangu wamemuhakikishia Mh Mavunde kuwa watakaa na wataalam wao wa Halmashauri na kuhakikisha wanatenga maeneo kwa ajili ya kutekeleza kilimo cha mkataba kupitia mfumo wa kizimba baina ya wakulima na mwekezaji huyo.

Share To:

Post A Comment: