Na Angela Msimbira TAMISEMI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Innocent Bashungwa ameonesha kuridhishwa na undikishwaji na kuripoti kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza huku akisisitiza kuwa Serikali imeanza mchakato wa kuajiri walimu na kuongeza matundu ya vyoo katika shule za umma.


Waziri Bashungwa ameyasema  hayo leo jijini Dodoma  wakati wa ziara ya kutembelea shule ya Sekondari ya Chamwino iliyoko katika Halmashauri ya  wilayani Chamwino Kwa lengo la kujionea wanafunzi walioripoti shule kwa wanafunzi wa kidato cha kwanza na msingi ambao wamenufaika na ujenzi wa madarasa 15,000.


Amesema baada ya Serikali kukamilisha madarasa kwa ajili ya kupokea wanafunzi wa kidato cha kwanza, Ofisi ya Rais-TAMISEMI imeanza mazungumzo na wizara ya utumishi kwa ajili ya kuajiri walimu sambamba na ujenzi wa matundu ya vyoo.


Aidha, amewaagiza wakuu wa Mikoa, Wilaya, wakurugenzi wa halmashauri  na maafisa elimu wa ngazi zote kuhakikisha wanasimamia kazi nzuri iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha wanafunzi waliofaulu wanaripoti shule na wenye umri wa kwenda shule wanaandikishwa sambamba na kusimamia miundombinu hiyo.


" Rais Samia amehakikisha kunakuwa na mahali pazuri pa kusomea kama hapa Shule ya Sekondari Chamwino, nielekeze wakuu wa mikoa, wilaya, wakurugenzi maafisa elimu ngazi zote wahakikishe wanafunzi waliofaulu wanaripoti shuleni na wale wenye umri wa kuanza shule waandikishwe."amesema  Waziri Bashungwa 


Aidha, Bashungwa ameziagiza halmashauri kuhakikisha inatumia sehemu ya mapato ya ndani kujenga nyumba za walimu sambamba na kupunguza sehemu ya fedha kutoka Serikali kuu kuelekeza katika ujenzi wa nyumba hizo lengo likiwa ni  kuweka mazingira mazuri.


" Sio hivyo tu pia Rais Samia anawajali walimu wake, hivyo  ni vyema kuhakikisha tunalinda na kutetea maslahi ya walimu ikiwemo kupandishwa madaraja."amesisitiza Waziri Bashungwa.


Amemuagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI  kuhakikisha maeneo yote ya Serikali zikiwemo shule, vituo vya afya na Hospitali za Wilaya kupimwa na kuatiwa hati ili kuwa na ulinzi na kuepusha uvamizi.

Share To:

Post A Comment: