Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizindua Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam tarehe 17 Desemba 2021

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akitoa maelekezo kwa Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya nchini Stela Tullo (Kushoto) wakati wa uzinduzi wa Baraza la Ardhi la Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam tarehe 17 Desemba 2021. Katikati ni Mkuu wa wilaya ya Kigamboni Fatma Almas Nyangasa.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza wakati wa uzinduzi wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam tarehe 17 Desemba 2021. Wa pili kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Kigamboni Fatma Almas Nyangasa na kulia ni Mbunge wa Jimbo la Kigamboni Dkt Faustine Ndugulile

Muonekano wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kigamboni lililozinduliwa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi.

************************

Na Munir Shemweta, WANMM

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya nchini kuepuka kuwapa Madalali amri za utekelezaji wa maamuzi katika mwisho wa siku za wiki na muda ambao siyo masaa ya kazi.

Hatua hiyo inafuatia kujitokeza kwa utoaji amri za utekelezaji wa maamuzi mwisho wa siku za wiki au baada ya masaa ya kazi jambo linalowanyima fursa walalamikaji kushiriki ama kukimbilia mahakamani kuzuia utekelezaji maamuzi.

‘’Kumekuwa na tabia ya baadhi ya Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba kutoa amri za utekelezaji maamuzi ya mahakama mwishoni mwa wiki kama siku ya ijumaa ambapo waislamu wako kwenye ibada na kuwanyima fursa ya kushiriki katika kesi huko ni kuwaonea wanyonge’’ alisema Lukuvi.

Waziri Lukuvi alisema hayo tarehe 17 Desemba 2021 wakati akizindua Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam kwa niaba ya Mabaraza mengine mapya 11 katika hafla iliyofanyika Kigamboni. Mabaraza yaliyozinduliwa ni pamoja na Mabaraza ya Ardhi na Nyumba katika wilaya za Ubungo, Kisarawe, Bagamoyo, Kasulu, Kibondo, Mwanga, Rombo, Mbogwe, Ludewa, Momba na Nkasi.

Kwa mujibu wa Lukuvi, tabia za kupiga mnada katika siku za mwisho wa wiki ambazo baadhi ya wananchi wanashiriki ibada ni kuwaonea wanyonge na kusisitiza kuwa ni vizuri Wenyeviti hao wakafuata sheria katika kutekeleza majukumu yao na kama ni maamuzi ya kupigwa mnada basi kazi hiyo ifanyike kwa uwazi na siku za kazi.

Alielekeza Wenyeviti wa Mabaraza ya Ardhi kukomesha pia tabia ya Madalali kuweka vijiwe kwenye ofisi za Mabaraza huku akitaka wale waliosajiliwa kufika katika ofisi hizo wakiwa na shughuli za kufanya kwa kuwa kumekuwa na tabia kwa baadhi yao kuzurura na kuwaongopea wananchi kuwa wanaweza kuwasaidia.

Lukuvi aliweka wazi kuwa, Serikali ipo katika hatua za mwisho za kutunga Kanuni za Madalali wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya zitakazowezesha uteuzi wa Madalalai wenye sifa sahihi kwa ajili ya utekelezaziji wa hukumu za Mabaraza.

Alisema, Kanuni hizo zitawezesha kuwepo ushirikiano baina ya Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Mahakama katika kusimammia Nidhamu na Maadili ya Maadili pamoja na kuwezesha uteuzi wa wajumbe wa kamati Madhubuti za Kusimammia Uteuzi, Nidhamu na Maadili ya Madalali katika ngazi ya Taifa, Mkoa na Wilaya.

Hata hivyo, Waziri Lukuvi alisema, tayari Serikali imeanza kuchukua hatua za kuweka kanuni hizo ili kukomesha matendo yanyovunja maadili aliyoyaeleza kuwa yamekuwa yakiwaiumiza sana wananchi.

Alisema, pamoja na Wizara ya Ardhi kuendelea kufanya juhudi mbalimbali za kuboresha utoaji huduma kwa Mabaraza bado Wenyeviti wanalo jukumu la kuwaelimisha wananchi ili wafahamu vizuri sheria, taratibu, na miongozo inayohusika katika kushughulikia mashauri ya ardhi.

Msajili wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya Wilaya nchini Stella Tulo alisema, uzinduzi wa Mabaraza 12 uliofanyika siyo tu utasaidia kupunguza mlundikano wa mashauri uliopo kwa baadhi ya Mabaraza bali yatawarahisishia wananchi kupata huduma iliyo karibu.

Kwa mujibu wa Stela Tullo, uzinduzi huo uliofanywa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi umewezesha Mabaraza kufikia wilaya 72 zenye Mabaraza yanayotoa huduma kati ya wilaya 139.

Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: