Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Prof. Maurice Mbago (wa pili kushoto) na Mjumbe wa Bodi ya TEA, Atupele Mwambene (watatu kushoto) walipowasili katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Nzovwe mkoani Mbeya. Aliyesimama kushoto ni Mkuu wa chuo hicho Silvanus Sitta.

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Prof. Maurice Mbago (katikati) akipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Silvanus Sitta (kulia). Aliyesimama kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa TEA, Bahati Geuzye.

Baadhi ya Wanufaika wa Mafunzo ya Kompyuta yaliyofadhiliwa na Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) katika Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Nzovwe wakiwa katika darasa la Kompyuta ambalo vifaa vyake vimenunuliwa kwa ufadhili wa SDF.

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Prof. Maurice Mbago, Mjumbe wa Bodi ya TEA Atupele Mwambene na maafisa wa TEA wakitembelea matanki ya kuzalishia Samaki katika Taasisi ya Ufugaji wa Samaki ya Riverbanks yaliyojengwa kwa ufadhili wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF).

Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Prof. Maurice Mbago (watatu kushoto) na Mjumbe wa Bodi ya TEA Atupele Mwambene (wa kwanza kulia) wakipata maelezo kutoka kwa wanufaika wa mafunzo ya ufugaji wa Samaki (hawako pichani).

Baadhi ya wanufaika wa Mafunzo ya kufuga Samaki kupitia Taasisi ta Ufugaji wa Samaki ya Riverbanks kwa ufadhili wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) wakiwa katika mabwawa yao ya kufuga Samaki walipotembelewa na wajumbe wa Bodi na maafisa kutoka Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA).

**********************

Wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) wameendelea na ziara ya kutembelea miradi inayofadhiliwa na TEA ambapo katika mkoa wa Mbeya wametembelea Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Nzovwe na Taasisi ya Ufugaji wa Samaki ya RiverBanks.

Taasisi hizo ni miongoni mwa Taasisi 81 zilizonufaika na ufadhili wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) kwa lengo la kuzijengea uwezo wa kutoa mafunzo ya ujuzi kwa vijana na akinamama ili waweze kuajiriwa au kujiajiri wenyewe.

Chuo cha Maendeleo ya Wananchi cha Nzovwe kilichopata ufadhili wa Shilingi Milioni 131 kupitia ufadhili wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi kimetoa mafunzo ya matumizi ya Kompyuta kwa wanufaika 396. Taasisi ya Riverbanks ilipata ufadhili wa Shilingi milioni 131 imetoa mafunzo ya ufugaji wa Samaki kwa wanufaika 420.

Mwenyekiti wa Bodi ya TEA, Prof. Maurice Mbago amekumbusha Taasisi hizo zilizonufaika na ufadhili wa SDF ambao ulihusisha ununuzi wa vifaa vya kufundishia kama kompyuta na vifaa vya uzalishaji wa Samaki kutunza vifaa hivyo ili viendelee kunufaisha wananchi wengi zaidi.

Kwa upande wao, wanufaika wa SDF katika Taasisi hizo wameishukuru Serikali kwa ufadhili huo ambao umesaidia hasa katika ununuzi wa vifaa vya kufundishia. Mkuu wa Chuo cha Nzovwe FDC Silvanus Sitta amesema idadi ya wanafunzi wanaojiunga na chuo imeongezeka kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya kujifunzia.

Aidha, Mkurugenzi wa Taasisi ya Ufugaji Samaki ya Riverbanks Pius Nyambacha amesema ufadhili wa SDF umewezesha kununua vifaa kadhaa ikiwa ni pamoja na vifaa vya kuzalishia vifaranga vya Samaki ambapo kwa sasa anawasambazia wafugaji wa Samaki walio karibu na Taasisi hiyo.

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ni Taasisi ya Umma inayofanya kazi chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. TEA inaratibu Mfuko wa Elimu wa Taifa na Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) unaofadhiliwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Dunia.
Share To:

emmanuel mbatilo

Post A Comment: