Mwandishi wetu,Arusha 


Timu ya mpira wa miguu ya wanaume ya bunge la Tanzania leo imemwaga misaada ya vifaa vya michezo kwa watoto wanaosakata soka katika kituo cha michezo cha Arusha Youth kilichopo jijini Arusha.


Misaada hiyo ni pamoja na seti ya jezi,mpira pamoja na soksi ambavyo vina thamani zaidi ya sh,2 milioni.


Akikabidhi zawadi hizo leo katika uwanja wa michezo wa kumbukumbu wa Sheikh Amri Abeid nahodha wa timu ya soka ya wabunge wa Tanzania,Cosato Chumi alisema kwamba lengo la kukabidhi zawadi hizo ni kuwapa hamasa na chachu watoto hao katika michezo hususani soka.


Chumi,ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Mafinga mjini alisema kwamba wao kama wabunge walijichanga na kutoa vifaa hivyo kama njia mojawapo ya kuchochea ari ya kukuza michezo nchini.


“Sisi kama wabunge tuliungana tukajichanga kama mchango wetu wa kukuza soka nchini kama sisi wabunge tunacheza soka kwanini watoto wasicheze “alisema Chumi 


Akipokea vifaa hivyo nahodha wa timu ya Arusha Youth,Atwai Shaban aliwashukuru wabunge hao na kuhaidi timu yao kufanya vizuri katika michezo hususani soka.


“Tunashukuru sana kwa hizi zawadi sisi tumefurahi sana kuona wabunge wametukumbuka “alisema Shaban 


Katika hatua nyingine timu ya mpira wa soka ya wabunge wa Tanzania imeendeleza wimbi la ushindi katika michuano ya mabunge wa Afrika Mashariki baada ya kuilaza timu ya taifa ya Kenya kwa mabao 2-1.


Mabao ya Tanzania yalifungwa kwa nyakati tofauti kipindi cha pili na wachezaji Abdallah Aman na Abdalla Moto na kuifanya Tanzania kuendeleza wimbi la ushindi katika michuano ya soka.


Michuano ya mabunge ya Afrika Mashariki inashirikisha nchi za Kenya,Uganda,Rwanda,Burundi,Sudan Kusini na wenyeji Tanzania ilifunguliwa mnamo Desemba 6 mwaka huu ambapo inataraji kuhitimishwa leo jijini Arusha ambapo Tanzania watafunga dimba kwa kukipiga na timu ya Taifa ya Sudani Kusini.

Share To:

Post A Comment: