Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mary Masanja (Mb) amehutubia kongamano kubwa la uwekezaji katika Sekta ya Utalii leo tarehe 12 Desemba, 2021 katika hoteli ya Shangri-la iliyopo Dubai.


Akiongea katika kongamano hilo Mhe. Masanja ameeleza nia ya kongamano hilo kuwa ni kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko nchini Tanzania pamoja na kujenga mahusiano ya kiuwekezaji kwenye Sekta ya Utalii.


“Kuna umuhimu mkubwa kutumia fursa ya maonesho haya ya Expo 2020 Dubai kutangaza na kuelezea fursa za uwekezaji zilizopo nchini.” Mhe. Masanja amefafanua na pia amewakaribisha wawekezaji kuwekeza kwenye Sekta hii nchini Tanzania.


Aliongeza kuwa, nchini Tanzania kuna fursa nyingi za uwekezaji katika maeneo ya mijini na sehemu mahsusi za utalii zikiwemo maeneo kiutamaduni na kihistoria, malazi yaani hoteli za kitalii, migahawa, maeneo ya michezo ya gofi, utalii ikolojia, utalii wa kumbi za mikutano na utalii wa uwindaji.


Kongamano hili limehudhiriwa na Mkurugenzi wa Idara ya Uchumi ya Diplomasia Dubai, Balozi  Edwin Rutageruka, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Allan Kijazi, Mtendaji Mkuu  wa Bodi ya Utalii nchini TTB, Betrita Lyimo, Bi. Hafsa Mbanga kutoka Kamisheni ya Utalii Zanzibar pamoja na Jumuiya ya Wafanyabiashara Dubai ikiwa ni sehemu ya Makongamano yaliyoandaliwa na Tanzania kwenye maonesho ya Expo 2020 Dubai.

Share To:

Post A Comment: