Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Balozi Ali Idi Siwa akizungumza wakati wa ufunguzi wa Baraza la 48 la Wafanyakazi wa NSSF lililofanyika Mkoani Tanga 
MKURUGENZI Mkuu wa NSSF Masha Mshomba akizungumza wakati wa ufunguzi wa Baraza la 48 la Wafanyakazi wa NSSF Mkoani Tanga 

Sehemu ya washiriki wa kikao hicho wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Masha Mshomba  katika akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa mfuko huo kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Balozi Ali Idi Siwa


Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Masha Mshomba  katika akiwa kwenye picha ya pamoja na watumishi wa mfuko huo kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF, Balozi Ali Idi Siwa


"Makusanyo ya Michango ya Wanachama Yaongezeka ,Thamani ya Mfuko yazidi Kukua.

NA OSCAR ASSENGA,TANGA


Ni habari njema! Unaweza kusema hivyo hasa kwa wanachama wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) kutokana na mwelekeo wa Mfuko huo kuzidi kuwa mzuri baada ya thamani ya Mfuko huo kukua na kufikia Shilingi trilioni 5.3 mwezi Novemba 2021.


Taarifa hizo njema kwa wanachama wa NSSF zilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo, Masha Mshomba wakati wa ufunguzi wa Baraza la 48 la wafanyakazi wa NSSF lililofanyika mkoani Tanga ambapo Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko huo, Balozi Ali Iddi Siwa alikuwa mgeni rasmi ikiwa ni kipindi chake cha pili cha kuiongoza bodi hiyo tangu alipoteuliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan


Mshomba alimhakikishia Balozi Siwa na wajumbe wa Baraza hilo kuwa, mafanikio hayo makubwa yametokana na ongezeko la makusanyo ya michango ya wanachama ambapo kwa mwezi yanafikia wastani wa Shilingi bilioni 105.


Alisema katika kipindi cha miezi mitano ya mwaka wa fedha 2021/22 hadi kufikia mwezi Novemba, mwaka 2021 wamefanikiwa kukusanya Shilingi bilioni 510 na kwamba wataendelea kukusanya zaidi ili waweze kutimiza malengo waliyojiwekea.


Mkurugenzi Mkuu huyo wa NSSF  alimpongeza Balozi Siwa kwa utendaji wake na amekuwa kiungo muhimu baina ya Menejimenti, Watumishi na Wizara inayosimamia sekta ya hifadhi ya jamii jambo ambalo limekuwa chachu ya mafanikio ya Mfuko huo.


Kwa upande wake, Balozi Siwa alisema katika kipindi cha miaka mitatu ya kwanza ya uongozi wa Bodi ya Wadhamini walifanikiwa kupata mafanikio ambayo yametokana na ushirikiano baina ya Wafanyakazi, Baraza la Wafanyakazi, Menejimenti, Bodi na Wizara inayosimamia sekta ya hifadhi ya jamii.

Mwenyekiti wa Bodi Balozi Ali Idi Siwa aliendelea kwa kusisitiza wajumbe wa Baraza kuongeza juhudi katika kusajili wanachama wapya katika sekta binafsi na kusimamia ukusanyaji wa michango kwa ufanisi zaidi, ongezeko la mapato kutoka uwekezaji hasa katika uwekezaji mpya kwenye maeneo salama, yenye tija na muda mrefu pamoja na kusimamia kwa umakini uwekezaji uliopo ili uweze kuleta matokeo mazuri na kupunguza gharama za uendeshaji.

Balozi Siwa alisema Mabaraza ya wafanyakazi yameundwa kisheria katika madhumuni ya kutoa ushauri katika ngazi za Wizara na taasisi zake kuhusu usimamizi wa kazi na rasilimali watu, utekelezaji wa majukumu wa kulinda haki na wajibu wa waajiri na wafanyakazi, kutoa ushauri kuhusu kujenga hali bora ya kazi katika kusimamia haki na ustawi katika sehemu za kazi.

Kwa upande wake, Mwakilishi kutoka Chama Cha Wafanyakazi wa Viwandani, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) na Mkuu wa Sekta za Taasisi za Fedha, Willy Kibona aliishukuru Menejimenti na wafanyakazi wote kwa ushirikiano kwamba wanaendelea kuzingatia kanuni na taratibu za sheria kama alivyoelekeza.


Share To:

TANGA RAHA BLOG

Post A Comment: